November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni ya NST Solution yachangia damu na kutoa vifaa tiba Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Wananchi wametakiwa kujitolea kuchangia damu katika vituo vya damu salama ili kupunguza changamoto ya uhaba wa damu kwa wenye uhitaji wa huduma hiyo.

Hayo ameyasema Mkurugenzi Mtendaji wa NST Solution Ramadhani Kiroboto wakati wakiadhimisha miaka 10 tangu kampuni yao ilipoanza, maadhimisho yaliyofanyika katika hospitali ya Rufaa Amana jijini Dar es Salaam ambapo wameshiriki zoezi la uchangiaji damu na kukabidhi vifaa mbalimbali vya kutolea huduma kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo ikiwemo vitambaa vinavyotumika katika upasuaji, vitanda vya kubebea wagonjwa n.k

Kiroboto amesema Uhaba wa damu na uhitaji wa damu ni mkubwa hivyo wale wote wanaoweza kuchangia wajitahidi kuja kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine.

“Leo tunasherehekea miaka 10 tangu kampuni hii ilipoanza na katika kusherehekea siku hii tukaona tujumuike na watanzania wenzetu kuja hapa hospitali ya rufaa ya Amana kwa kutoa msaada wa vifaa na kushiriki katika uchangiaji wa damu”

“Tuliona katika kuadhimisha miaka 10 ya kampuni na kurudisha kwa jamii kwa kile ambacho wamekua wakituunga mkono kwa miaka yote 10 tuje turudishe kwa jamii kupitia mchango wa vifaa lakini pia mchango wa damu salama kwaajili ya mahitaji ya wagonjwa” Amesema Kiroboto.

Kiroboto ameushukuru uongozi wa hospitali ya Amana kwa kuruhusu kwenda kushirikiana nao hivyo aliwahamasisha wadau wengine kwenda kuchangia damu na kutoa vifaa tiba.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma saidizi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Amana, Mfamasia Onoratha Chagula ameishukuru kampuni ya NST Solution kwa kuwapa vifaa hivyo kwani vinamanufaa sana katika kutolea huduma hospitalini hapo.

“Tunashukuru sana kwa msaada tulioupata, Hospitali ni eneo ambalo lipo maalum kwaajili ya huduma za kimatibabu ikiwa ni pamoja na kuokoa maisha ya wananchi hivyo katika kazi zetu za Kilasiku huwa tunatumia vifaa hivi tulivyoletewa leo”.

Kwa upande wa damu, Chagula amewashukuru sana NST Solution kwa kuchangia damu hospitalini hapo lakini pia aliwakaribisha wananchi wengine kuchangia damu kwa wingi kwani uhitaji wa damu ni mkubwa, ili waweze kuokoa maisha ya mwananchi mwingine.