November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jafo,Exim na Habari Development Association washerekea Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupanda miti

Na Joyce Kasiki,Timesamajira online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo  ameungana na wadau wa mazingira kusherekea maadhimisho ya 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo huadhimishwa Januari 12 ya kila mwaka kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma.

Shughuli hiyo ya upandaji miti imeratibiwa na Taasisi ya Habari Development Association kwa kushirikiana na  Benki ya Exim Tanzania .

Akizungumza mara baada ya shughuli ya kupanda miti katika solo la Machinga Complex  jijini Dodoma Dkt. Jafo amesema 

 Wizara yake kwa kushirikiana na wadau hao imejipanga kutumia vema Maadhimisho hayo kwa kuendesha jitihada mbalimbali za utunzaji mazingira hususan kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali nchini.

“Jambo hili lililofanywa na Benki ya Exim na Habari Association ni la kuigwa ,kwani wameungana na   serikali ili kufanikisha zoezi hili muhimu ambalo ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 59 tangu kufanyika kwa Mapinduzi Zanzib,nachukua nafasi hii kuwaongeza na kuwashuru sana wadau hawa.”amesema Dkt.Jafo na kuongeza kuwa 

“Taifa kwa sasa  linapitia changamoto nyingi zinazotokana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kusababisha upungufu wa mvua kwa karibu nusu ya kiwango kilichozoeleka na kwamba hatua hiyo imesaababisha upungufu wa uzalishaji wa chakula, upatikanaji wa huduma ya maji, ukosefu wa umeme wa uhakika na hivyo kusababisha kuporomoka kwa uchumi.”

Ofisa Mkuu Idara ya Fedha wa EXIMShani Kinswaga akipanda mti katika soko la Machinga jijini Dodoma

Hata hivyo amesema serikali inaendelea na miradi mbalimbali inayolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo miradi mbalimbali inayolenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa, kuchimba mabwawa makubwa ya kuhifadhi maji sambamba na mradi wa uzalishaji umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere zote hizi zikiwa ni jitihada za kuhakikisha kama taifa hatuathiriki sana na changamoto hii.

Ofisa Mkuu Idara ya Fedha (CFO) Benki ya Exim Shani Kinswaga amesema benki hiyo imekuwa ikiunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kuja na namna mbalimbali ikiwemo kupitia Program yake ya ‘Exim Go Green Initiative’ kwa kuhamasisha upandaji wa miti na utunzaji mazingira nchini kupitia matawi yake yaliyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Amesema ,kwa upande wa ukanda  wa kati, jiji hili la Dodoma limebahatika kuwa chaguo la Benki ya Exim katika kuendesha Programu hii na kwamba zoezi hili ni la tatu kwa benki ya Exim kushiriki katika kipindi cha miaka mitatu katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.

Kwa mujibu wa  Kinswaga, benki hiyo kama taasisi ya fedha nchini inaguswa pia na chanagmoto za kiuchumi zinazotokana na athari ya mabadiliko ya tabia nchini hivyo imedhamiria kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazolenga kukabiliana na changamoto hiyo.

Awali akizungumza kwenye tukio hilo, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Habari Development Association Bernard Mwanawile amesema taasisi yake imejipanga kupanda miti milioni Moja mkoani humo.

Mwanawile ametumia nafasi hiyo  kuwapongeza wadau mbalimbali wanaounga mkono mpango huo wa kupanda miti  ikiwemo benki ya Exim ambayo hadi sasa imeweza kufadhili upandaaji wa miti 16,000.

Naye Meneja wa Soko la Machinga Complex Veronica Tarimo aliahidi kuhakikisha kwamba soko hilo na wadau wake wote wakiwemo wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara zao kwenye soko hilo wataitunza vema miti hiyo sambamba na kuendelea na mkakati wao wa utunzaji mazingira katika soko hilo.

Ametumia nafasi hiyo kuiomba benki ya Exim iweke kambi kwenye soko letu ili itoe elimu ya kifedha kwa wafanyabiashara ndani ya soko hilo na kuwapatia mikop kwa ajili ya kukuza biashara zao.