November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miradi ya kimkakati ya zaidi ya Bil 11 kutekelezwa Ngara

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Ngara

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera inatarajia kunufaika na miradi 9 itakayotekelezwa kupitia program ya NELSAP (Nile Equatorial Lake Subsidiary Action Program) ambao ni Wasimamizi Wakuu wa Mradi wa Uzalishaji Umeme unaotekelezwa katika Bwawa la Rusumo.

Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Solomon Kimilike alisema miongoni mwa miradi itakayotekelezwa kupitia program hiyo ni ujenzi wa Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya hiyo na soko la kimkakati litakalojengwa mpakani, katika Kijiji cha Kahaza-Rusumo.

Alitaja miradi mingine ya kimkakati itakayotekelezwa kuwa ni ujenzi wa jengo la kisasa la maegesho ya magari makubwa ya mizigo yanayoelekea nchi jirani za Burundi, Rwanda, DR Congo na Uganda kupitia Wilaya hiyo.

Alibainisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kutokana na makubaliano maalumu na NELSAP ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa jamii inayozunguka mradi huo mkubwa wa kufua umeme katika Bwawa la Mto huo.

Aliongeza kuwa miradi yote itakayotekelezwa kupitia program hiyo inafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) ambapo gharama za ujenzi pamoja na usimamizi wake zinatarajiwa kufikia dola za kimarekani mil 5, ambazo ni sawa na sh bil 11.5.

Kimilike alitaja miradi mingine kuwa ujenzi wa mabweni, ukumbi na bwalo la chakula katika shule ya sekondari Ngara na ukarabati wa barabara ya kuunganisha Kituo cha Afya Rusumo kwa kiwango cha lami na ujenzi wa uzio wa Kituo hicho.

Mingine ni ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kati kuunganisha Kituo hicho cha afya na kuunganisha mradi wa maji Rusumo huku nyingine ikitarajiwa kuunganisha shule ya sekondari Ngara (high school).

Alisisitiza kuwa utekelezaji miradi hiyo unataraqjiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka 2023 na kumalizika mwishoni mwa mwaka huo, kwa sasa halmashauri ipo katika maandalizi ya kupata wakandarasi na wakandarasi washauri.

Alitaja matarajio yao kupitia miradi hiyo kuwa ni kuongeza pato la halmashauri, kuongeza pato la wananchi wanaoishi karibu na miradi hiyo, kukuza eneo la Rusumo, kukuza mahusiano na nchi jirani na kuongeza usalama wa mali na vifaa kwa wafanyabiashara wa magari makubwa watakaotumia maegesho ya Benaco.

Alisema miradi hiyo inatarajiwa kutekelezwa katika vijiji vya Rusumo, Kahaza na Mumasama katika halmashauri ya wilaya hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera Solomon Kimilike akifafanua miradi itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia program ya NELSAP ambayo ni ujenzi wa Jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya hiyo, soko la kimkakati na gereji kubwa ya magari ya mizigo. Picha na Allan Vicent