January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LATRA kukutana TIRA kujadili utaratibu wa abiria kulipwa pindi wanapoumia inapotokea ajali

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri nchini (LATRA) inatarajia kukutana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) kwa ajili ya kuzungumzia suala la ulipwaji bima ya majeruhi wa ajali pale zinapotokea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Hayo yamesema na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habibu Suluo akati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kupanda kwa nauli za mabasi yaendayo haraka jiji Dar es Salaam ambapo pia alitoa utaratibu wa nauli za bajaji na pikipiki Mtandao.

“Inapotokea ajali na abiria wakaumia au kufariki,hao wote wanapaswa kulipwa na mmiliki wa basi husika kwa sababu magari yao wameyakatia bima na suala hilo lipo kisheria ,lakini mara nyingi hilo huwa halifanyiki ,unakuta mtu kaumia kwenye ajali ya basi lakini halipwi chochote.”amesema CPA Suluo

Amesema hali hiyo imewafanya kuandaa kikao cha pamoja na TIRA ili kuzungumza na kuliweka sawa jambo hilo ili abiria waweze kupata haki zao pindi inapotokea ajali.

“Baada ya kukutana na TIRA tutatoa taarifa kwa umma ili jamii iweze kufahamu na kudai haki yao ya msingi pindi wanapoumia katika ajali za mabasi.”amesisitiza

Amesema wamekuwa wakipigia kelele suala hilo lakini wameona halitekelezwi ndio maana wameamua kukaa kikao ili kuwekeana mikakati ya kuhakikisha kila mmoja anajua sheria hiyo.

Akizungumzia kuhusu tiketi mtandao ameiasa jamii kuhakikisha wanapewa tiketi ambazo zina majina kamili pamoja na namba za simu ili waweze kupata haki ya fidia pindi inapotokea ajali.

Kwa mujibu wa CPA Suluo kila tiketi abiria anayopewa abiria  anapaswa kuikagua ili kuona kama taarifa zake zipo sahihi yakiwemo majina kamili .