November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kumega Hekta 33,132.24 za hifadhi kuwapatia wananchi Ruvuma

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali itamega jumla ya hekta 33,132.24 katika mkoa wa Ruvuma kutoka maeneo ya hifadhi na shamba la NAFCO na kubakizwa kwa wananchi kwa ajili ya matumizi mbalimbali.Aidha, imeelekeza wananchi wote waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Lihanje uliopo halmashauri ya wilayani Songea kusitisha shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo ya mlimani na bondeni mwaka huu,

Hayo yameelezwa tarehe 30 Desemba 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula katika kikao cha Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta na uongozi wa mkoa wa Ruvuma wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara kwa ajili ya kutoa mrejesho wa Maamuazi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na Utatuzi wa Migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji 975.

Dkt Mabula ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta alisema, mkoa wa Ruvuma unahusisha vijiji/mitaa 38 yenye migogoro ya matumizi ya ardhi ambapo maamuzi ya Kamati ni kumega sehemu ya maeneo ya hifadhi kuwaachia wananchi sambamba na kusitishwa shughuli za kibindamu kwenye hifadhi .

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, wakati wa zoezi la tathmini kuhusu migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye mkoa wa Ruvuma timu ya wataalamu ilivifikia vijiji/mitaa 38 katika wilaya za Mbinga, Nyasa, Tunduru, Namtumbo na Songea ambapo zoezi la uwandani lilihusisha na kufanya vikao na uongozi wa serikali za vijiji husika na kisha kutembelea maeneo yenye migogoro.

‘’Pamoja na maamuzi haya ya serikali ya kumega maeneo kwa ajili ya vijiji mkoa unalo jukumu la kusimamia utekelezaji wa maamuzi hayo kwa kusimamia utekelezaji huo kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka zote zilizopo ndani ya mkoa na ni muhimu maeneo haya yaliyomegwa kuandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi ili kuepuka matumizi holela ’’ alisema Dkt Mabula.

Akigeukia umauzi wa serikali kusitisha shughuli za kibinadamu kwa wananchi waliovamia hifadhi ya msitu wa Lihanje, Dkt Mabula ameelekeza mkoa kwa kushirikiana na timu atakayoiunda kufanya tahmini ya kina ya mahitaji halisi ya ardhi kulingana na idadi ya watu waliopo katika vijiji hivyo na kuahidi timu yake ya mawaziri wa wizara za kisekta kurejea tena mapema januari 2023 kwa ajili ya kupokea taarifa na kutoa maamuzi.

’wananchi wote waliovamia hifadhi yam situ wa Lihanje kwa kuendesha shughuli za kilimo kwa maeneo ya mlimani na bondeni wanaelekezwa kusitisha shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo hayo kwa mwaka huu’’ alisema Dkt Mabula.

Msitu wa Lihanje unasimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na ni vyanzo muhimu vya maji vyenye mradi wa maji mtiririko Luyelela na Kilagano ambapo wananchi wamevamia takriban asilimia 60 ya msitu na kuendesha shughuli za kilimo,

Aliushukuru mkoa wa Ruvuma kwa kuweza kuratibu vyema zoezi la tahmini alilolieleza kuwa limewezesha kazi hiyo kufanyika kwa amani na utulivu huku akitambua mkoa huo unazo changamoto nyingi zinazosababishwa na muingiliano wa matumizi ya ardhi.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana amewataka wananchi kukemea wale wanaoharibu vyanzo vya maji na kuzitaka mamlaka zote kuanzia ngazi ya vijiji kuhakikisha zinadhibiti uvamizi wowote unaofanyika katika hifadhi za misitu na mapori ya akiba.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Comredi Odo Mwisho amesema chama chake kinaungana na serikali kuhakikisha inalinda maeneo yote yaliyotamkwa kuwa ni hifadhi ya asili ili kuepuka uharibifu wa mazingira n auto wa asili.

Timu ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta imehitimisha ziara yake katika mkoa wa Ruvuma na januari nne , 2023 inatarajiwa kuendelea na ziara yake katika mkoa wa Mara.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza katika kikao baina ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta na uongozi wa mkoa wa Ruvuma tarehe 30 Desemba 2022.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza katika kikao baina ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta na uongozi wa mkoa wa Ruvuma tarehe 30 Desemba 2022. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana na kulia ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.
Sehemu ya washiriki wa kikao baina ya Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta na uongozi wa mkoa wa Ruvuma tarehe 30 Desemba 2022.
Mawaziri wa Wizara za Kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa tatu kulia) wakiondoka mkoani Ruvuma baada ya kumaliza kazi ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika mkoa huo 30 Desemba 2022.