November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Chacha akasirishwa na vitendo vya rushwa ajira za SGR

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MKUU wa Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa wilaya ya Tabora Mjini Paul Chacha ameuagiza uongozi wa Kampuni ya Yapi Merkez inayojenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Makutopora Dodoma hadi Tabora kuwaondoa mara moja wakuu wa vitengo vya ajira, usaili na afya wanaotuhumiwa kuomba rushwa kwa vijana wanaomba kazi katika kampuni hiyo.

Ametoa agizo hilo katika kikao cha pamoja baina ya Uongozi wa Kampuni hiyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Tabora Mjini kilichofanyika katika Ofisi za Kampuni hiyo.

Alisema vijana wengi hususani wakazi wa Mkoa huo wamekuwa wakilalamikia vitendo hivyo ambavyo vimepelekea wengi wao kukata tamaa ya kupata ajira katika mradi huo licha ya serikali kuagiza miradi hiyo kunufaisha wazawa.

Ili kumaliza kero hiyo aliagiza Uongozi wa Kampuni hiyo kuwaondoa watumishi wote wanaolalamikiwa kuendekeza vitendo hivyo kwa vijana wa Kitanzania ili wapate kazi.

Alisisitiza kuwa serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyasika kupata ajira wakati Mkandarasi huyo anahitaji wafanyakazi wazawa wengi katika mradi huo mkubwa hapa nchini.

‘Tumepokea malalamiko mengi toka kwa vijana wetu ya kuombwa rushwa ya sh laki 2 na nusu hadi 3 ili kuajiriwa na kampuni hiyo inayotekeleza mradi huo’, alisema.

Kamimu mkuu huyo wa wilaya ya Tabora aliwataka vijana na wananchi kwa ujumla wanaofika kupata ajira katika kampuni hiyo watoe taarifa kwa serikali pindi atatokea mtu kuwaomba rushwa.

DC Chacha alisema anazo taarifa za Watumishi 9 wa Kampuni hiyo wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kuwaomba rushwa vijana ili wapate ajira hizo, hivyo akaelekeza wasakwe na kuondolewa.

Alibainisha hao wanataka kuharibu sifa nzuri ya Kampuni hiyo ya Kimataifa ili ionekane haifai hivyo akaagiza wananchi kutoa taarifa kwa serikali pale watakapokutana na changamoto hiyo ya kuombwa rushwa.

Aidha katika kikao hicho DC alishauri kampuni hiyo kuweka rangi kwenye mafuta wanayoagiza ili inapotokea hujuma yoyote ya wizi wahusika waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua ili kupunguza wizi wa mafuta unaofanywa na madereva wa mitambo na magari.

Hatua hiyo inafuatia jeshi la polisi mjini Tabora kukamata mafuta dumu 64 zenye ukubwa lita ishirini kila moja pamoja na watuhumiwa tisa akiwemo dereva mmoja wa kampuni ya Yapi Merkezi akihusishwa na wizi huo. Ambao wanasubiri kufikishwa mahakamani.

Akiongea katika kikao hicho Meneja mradi kutoka Kampuni ya Yapi Merkezi Gokhan Ginar alisema wapo tayari kumfukuza kazi mtu yoyote atakayebainika kuhusika na tuhuma za rushwa katika ajira.

Kuhusu wizi wa mafuta alisema wamekuwa wakijaza mafuta kwenye magari ili iwe rahisi kwao kubaini kama wanahujumiwa na kwamba wamepokea ushauri wa serikali na wataufanyia kazi.

Naye Mhandisi Ayubu Mdachi ambaye ni Meneja wa Mradi huo wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) alisema hadi sasa ujenzi wa reli hiyo umefikia asilimia 3.

Aliongeza kuwa hadi sasa jumla ya vijana na watu wazima walioajiriwa ni 2,993 kati ya watu 7,000 ambao wanatarajiwa kupata ajira katika vitengo mbali mbali.