November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri ya Ngara yatoa mikopo zaidi ya Mil.626

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Ngara

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera imetoa mikopo nafuu isiyo na riba ya jumla ya sh mil 626.5 kwa vikundi 72 vya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na ujasiriamali ili kuwainua kiuchumi.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Solomon Kimilike, Kaimu Mkurugenzi Josephat Sangatati alisema mikopo hiyo imewezesha wananchi wengi kujiongezea kipato.

Alisema fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani ya halmashauri ambapo serikali ilielekeza asilimia 10 ya mapato hayo kutolewa kwa vikundi vya wajasiriamali kwa mgawanyo wa asilimia 4 kwa vijana, 4 kwa wanawake na 2 kwa walemavu.

Alibainisha vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2021/2022 kuwa ni 42 vya wanawake vilivyopewa mil 309.3, vya vijana 23 vilivyopata mil 286.9 na 6 vya walemavu vilivyopewa mil 30.2.

Sangatati alifafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 pekee walitoa sh mil 132.5 kwa vikundi 27, mwaka wa fedha 2020/2021 wakatoa sh mil 169.1 kwa vikundi 13 na mwaka wa fedha 2021/2022 wametoa sh mil 324.9 kwa vikundi 32.

‘Tunatoa mikopo hii ili kutekeleza agizo la serikali la kuinua wananchi kiuchumi na ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025’, alisema.

Alibainisha kuwa utoaji mikopo hiyo isiyo na riba umesaidia sana jamii kupambana na umaskini wa kipato kwani wanavikundi wengi wameweza kuongeza vipato vyao hivyo kuboresha maisha yao.

Ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na mikopo hiyo alisema halmashauri kupitia Idara yake ya Maendeleo ya Jamii imeendelea kufuatilia utendaji wa vikundi hivyo na kukusanya marejesho ya mikopo yao.

‘Hadi sasa sh mil 379.2 zimerejeshwa kati ya mil 420.2, kwa mwaka 2019/2020 pekee walirejesha mil 129.9 baki mil 2.5, mwaka 2020/2021 walirejesha mil 130.5 baki mil 38.4 na mwaka 2021/2022 wamerejesha mil 118.7 baki mil 206’, alisema.

Kaimu Mkurugenzi alibainisha kuwa changamoto ya baadhi ya vikundi kutorejesha mikopo yao imeendelea kushughulikiwa ili kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati na kwa wale wasiorejesha kufunguliwa shauri la madai mahakamani.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya wilaya ya Ngara Mkoani Kagera Emanuel Kulwa (wa kwanza kushoto aliyevaa koti) akiwa katika picha ya pamoja na Kikundi cha Wajasiriamali cha Kabanga Chalk Group kinachojishughulisha na uzalishaji chaki na mbao za gipsamu baada ya kutembelea kiwanda hicho hivi karibuni kujionea jinsi wanavyozalisha biadhaa hizo, kikundi hicho kilikopeshwa sh mil 15 mwaka jana na kimerejesha zote. Picha na Allan Vicent.