November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wa Hale wapata kituo cha afya

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

WANANCHI wa mji mdogo wa Hale katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, hatimaye wamepata kituo cha afya baada ya majengo yaliyokuwa kambi ya watengeneza barabara ya kutoka Tanga- Chalinze kampuni ya SBI kugeuzwa kituo cha afya.

Jitihada za majengo hayo kuwa Kituo cha Afya Hale ni jitihada za Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini (CCM) Timotheo Mnzava, Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, na wananchi wa Hale.

Akizungumza Desemba 24, 2022 na wananchi wa Kijiji cha Hale waliofika kufanya msalagambo wa kufanya usafi kwenye eneo hilo, Mnzava alisema haikuwa kazi rahisi eneo kuwa kituo cha afya sababu, tayari halmashauri ilishachukua eneo hilo mara baada ya kazi ya utengenezaji barabara kukamilika zaidi ya miaka 10 iliyopita, na kufanya chanzo cha mapato.

Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ilikodisha majengo hayo ambapo makubwa ni manne (4), kwa baadhi ya wafanyakazi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima, Uganda kwenda Chongoleani, Tanga.

“Nilipoingia kwenye ubunge 2018 nilikuta majengo yamekodishwa.

Mwaka 2019 niliomba na kushawishi na kueleza nia yangu ya kutaka majengo hayo yatoe huduma za jamii, nikaelezwa bado yana mkataba.”

“Halmashauri walikuwa wamekodisha. Mimi na Diwani wa Kata ya Hale Mhidini Rajab hilo lilikuwa deni kwetu, na mwisho wa siku tumekatisha mkataba na wale watu tumefanikiwa kuwaondoa.”

“Sasa hatua ya pili ni kubadilisha matumizi, na tulichochagua ni kufanya eneo hili kuwa Kituo cha Afya Hale. Tumejenga Kituo cha Afya Mnyuzi katika Kijiji cha Mkwakwani, lakini tumeona kule ni kama kushoto kwa wananchi wa Kata ya Hale uwaeleze waende Mnyuzi.Hivyo Kituo cha Afya Mnyuzi kitabaki kuhudumia wananchi wa Kata ya Kwagunda na Mnyuzi, na Hale ni lazima iwe na kituo chake cha afya, na hiyo ni kutokana na jiografia” alisema Mnzava.

Mnzava alisema wanafanya jitihada Kituo cha Afya Hale kianze Januari, 2023, na kutaka wataalamu hasa Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri aweze kufika hapo kabla ya Januari 10, 2023 afanye tathmini ya kufanya ukarabat wa majengo hayo.

Mnzava alisema wakati wananchi wanaendelea kutoa michango kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo, yeye atafanya jitihada ya kujengwa jengo muhimu la kabla na baada ya mama kujifungua ambalo ndani yake litakuwa na huduma za upasuaji ambalo ujenzi wake utagharimu sh. milioni 250. Na kwa kuanzia, yeye atatoa sh. milioni tano kwa ajili ya ukarabati wa majengo yaliyopo ili huduma ianze Januari, 2023.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe alisema waliona kutoa majengo hayo kuwa Kituo cha Afya Hale ni bora kuliko mapato wanayopata kupitia kukodisha majengo hayo. Hivyo kama halmashauri, wao watatoa sh. milioni tano kufanikisha ukarabati, na kituo hicho kianze kazi haraka iwezekanavyo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Ally Waziri alisema haikuwa kazi rahisi kwa halmashauri kutoa eneo hilo kuwa kituo cha afya sababu tayari ilikuwa ni chanzo chake cha mapato.

Lakin madiwani walisema afadhali wakose mapato, lakin wananchi wapate huduma za jamii, huo ni uzalendo wa hali ya juu.

“Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020- 2025, hivyo viongozi wote wa ngazi zote, tuwe tayari kuwa wa kwanza kutekeleza ilani. Wamama wa Hale wanaenda kujifungua Kituo cha Afya Majengo kilichopo Halmashauri ya Mji Korogwe, hivyo ni muhimu wamama wakajifungulia hapa. Nataka hadi Januari 10, 2023 Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri na wataalamu wengine ikiwemo umeme na maji, wawe wameshaweka tathmini ya gharama za ukarabati kwenye majengo haya” alisema Waziri.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Dkt. Miriam Cheche alisema majengo hayo manne yaliyopo eneo hilo yanaweza kuanza kwa Wagonjwa wa Nje (OPD), maabara na huduma jingine, lakini kuna jengo muhimu sana lazima lijengwe la wodi ya mama kabla na baada ya kujifungua, ambapo ndani kuna huduma ya upasuaji, na linagharimu sh. milioni 250.Diwani wa Kata ya Hale Mhidini Rajab, alisema waliomba hayo majengo ya SBI kwa huduma za jamii, na sio kuweka kiwanda cha machungwa ama mkonge, na wakaweza kuyapata.

Rajabu alisema awali walikuwa wajenge kituo cha afya kipya, huku kila mwananchi wa Kata ya Hale akitakiwa kuchangia sh. 35,000, lakini kwa kupata majengo ya SBI, sasa wanaweza kupunguza michango kutoka sh. 35,000 kwa mtu mmoja hadi sh. 10,000 ama sh. 5,000 kwa mtu mmoja.

Baadhi ya majengo yaliyopo Kata ya Hale, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, ambayo yalikuwa ofisi za Kampuni ya SBI iliyokuwa inatengeneza barabara ya Tanga- Chalinze, ambayo kwa sasa yamebadilishwa matumizi, na yatakuwa Kituo cha Afya Hale. (Picha na Yusuph Mussa).
Baadhi ya majengo yaliyopo Kata ya Hale, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, ambayo yalikuwa ofisi za Kampuni ya SBI iliyokuwa inatengeneza barabara ya Tanga- Chalinze, ambayo kwa sasa yamebadilishwa matumizi, na yatakuwa Kituo cha Afya Hale. (Picha na Yusuph Mussa).
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe (katikati) akikagua moja ya majengo yaliyopo Kata ya Hale, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, ambayo yalikuwa ofisi za Kampuni ya SBI iliyokuwa inatengeneza barabara ya Tanga- Chalinze, ambayo kwa sasa yamebadilishwa matumizi, na yatakuwa Kituo cha Afya Hale. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na Diwani wa Kata ya Hale, Mhidini Rajab, na kulia ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Hale Zahara Omar. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini (CCM) mkoani Tanga Timotheo Mnzava (wa pili kushoto), akizungumza na wananchi wa Kata ya Hale. Ni baada ya kufika kwenye majengo yaliyokuwa ofisi za Kampuni ya SBI iliyokuwa inatengeneza barabara ya Tanga- Chalinze ili kufanya usafi katika majengo hayo baada ya kubadilishwa matumizi na kuwa Kituo cha Afya Hale. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Diwani wa Kata ya Hale Mhidini Rajab. (Picha na Yusuph Mussa).
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Ally Waziri (wa tatu kushoto), akizungumza na wananchi wa Kata ya Hale. Ni baada ya kufika kwenye majengo yaliyokuwa ofisi za Kampuni ya SBI iliyokuwa inatengeneza barabara ya Tanga- Chalinze ili kufanya usafi katika majengo hayo baada ya kubadilishwa matumizi na kuwa Kituo cha Afya Hale. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe. (Picha na Yusuph Mussa).
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe (DMO) Dkt. Miriam Cheche, akizungumza na wananchi wa Kata ya Hale. Ni baada ya kufika kwenye majengo yaliyokuwa ofisi za Kampuni ya SBI iliyokuwa inatengeneza barabara ya Tanga- Chalinze ili kufanya usafi katika majengo hayo baada ya kubadilishwa matumizi na kuwa Kituo cha Afya Hale. (Picha na Yusuph Mussa).