November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi zaidi ya 10,000 kunufaika na maji Lushoto

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto

MRADI wa Maji wa Irente- Yoghoi- Ngulwi- Bombo uliopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, unatarajia kunufaisha wananchi 6,239 kwenye vijiji takribani vinne, na kuondoa adha ya maji kwenye maeneo hayo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Desemba 21, 2022, mara baada ya Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo kufanya ziara ya kukagua miradi ya maji Lushoto, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Kayetan alisema hadi kukamilika mradi huo utagharimu sh. milioni 578,175,639.

Kayetan alisema mradi huo unahusisha vilula (vituo vya kuchotea maji) 17, ukarabati wa matenki mawili yenye ujazo wa lita 175,000 kila moja na jingine la lita 50. Pia ujenzi wa chanzo kipya, na ulazaji wa bomba mita 13,500.

“Mradi wa Maji wa Irente-Yoghoi-Ngulwi-Bombo utanufaisha wananchi 6,239. Ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu sh. milioni 578,175,639, na utakuwa na vilula 17, ukarabati wa matenki mawili ya lita 175,000 kwa kila moja na tenki lingine la lita 50. Ujenzi wa chanzo kipya, na
ulazaji wa bomba umbali wa mita 13,500 chini ya Mkandarasi Buzubona & Sons Company Ltd wa Karagwe, Kagera. Mkataba unaisha mwishoni mwa mwezi Januari, 2023″ alisema Kayetan

Kayetan alisema kwenye Mradi wa Maji wa Funta katika Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto utakuwa na vilula 23, na wakazi 4,782 watanufaika, na utagharimu sh. 832,655,200 hadi kukamilika kwake. Pia utahusisha ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 90,000 ujenzi wa chanzo kipya, na ulazaji wa bomba mita 9,900, huku Mkandarasi akiwa ni KOBERG Construction ltd, mkataba unaisha mwishoni mwa Mei, 2023.

Mhandisi Lugongo alimuhakikishia Diwani wa Kata ya Ngulwi Edwin Shunda kuwa RUWASA wapo tayari kuongeza mahitaji ya matenki kwenye kata hiyo, ili mradi wananchi wachangie gharama ya maji ili miradi iwe endelevu.

Mhandisi Lugongo aliweka msisitizo juu ya utunzaji maznngira, na kulinda vyanzo vya maji, hasa Kata ya Funta ambapo ameona maeneo mengi yameharibiwa kutokana na uchimbaji madini, hivyo anaamini viongozi wa vitongoji, vijiji, kata na wilaya watakaa kuweza kuweka mikakati ya kulinda vyanzo vya maji na mtiririko wa maji yanakopita.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo akipanda juu ya tenki la maji lililojengwa kwenye Kata ya Ngulwi, Wilaya ya Lushoto. (Picha na Yusuph Mussa).
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (kushoto), akiteta jambo na Diwani wa Kata ya Ngulwi, Wilaya ya Lushoto Edwin Shunda (kulia), na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Kayetan (katikati). Ni baada kufika kukagua tenki la maji lililofanyiwa ukarabati kwenye kata hiyo. (Picha na Yusuph Mussa).
Moja ya tenki lenye ujazo wa lita 175,000 lililofanyiwa ukarabati kwenye Kata ya Ngulwi, Wilaya ya Lushoto. (Picha na Yusuph Mussa).
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (wa pili kulia) akikagua tenki la maji linalojengwa Kata ya Funta, Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto. Kulia ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Kayetan (Picha na Yusuph Mussa).
Baadhi ya mashimo yaliyoachwa na wachimba dhahabu kwenye Kata ya Funta, Halmashauri ya Bumbuli, wilayani Lushoto. Uchimbaji huo wa madini unaathiri mtiririko wa maji kupita kwenye njia yake. Na huenda baada ya miaka mitano hadi 10 vyanzo vya maji vikakauka wilayani humo, na kuathiri upatikanaji wa maji kwa miradi inayojengwa na Serikali. (Picha na Yusuph Mussa).