Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete ameitaka Wizara yake kupitia ofisi za Kamishna wasaidizi wa ardhi nchini kufanya uhamasishaji kwa wananchi ili wajue umuhimu wa kuchukua hatimiliki za ardhi.
Ridhiwani amesema hayo desemba 22, 2022 mkoani Dar es Salaam wakati akifungua mkutano baina ya ofisi ya kamishna msaidizi wa ardhi mkoa wa Dar es salaam na makampuni yanayofanya kazi katika miradi ya urasimishaji makazi holela kwa lengo la kutatua changamoto za urasimishaji katika mkoa huo.
“Kama ninyi mtaona kazi yenu inaishia katika kufanya usajili wa michoro ya mipango miji na kuwawekea mawe wananchi mkaamini mmemaliza kazi hii haitoshi,mnachotakiwa ni kuwa na kazi ya kufanya ya kuhamasisha wananchi kuchukua hati”. Alisema Ridhiwani.
Ridhiwani ameelezea tofauti kubwa kati ya idadi ya viwanja vilivyopandwa mawe katika mkoa wa Dar es Salaam na vile vilivyotolewa hati na kuielezea hali hiyo kuwa hesabu zake zinakataa kabisa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi idadi ya viwanja vilivyopandwa mawe katika mkoa wa Dar es Salaam ni 238,800 na viwanja vilivyopimwa na kuidhinishwa 106,000 huku vilivyotolewa hati ni 24,000 jambo ambalo halileti afya katika sekta ya ardhi.
“Kama tunaweza kuwa na viwanja 238,800 vinavyotakiwa kulipiwa huku viwanja 24,000 pekee vikilipiwa basi hapo kuna tatizo na hapa ni nani wa kuwaambia wananchi umuhimu wa kuwa na hatimiliki ya ardhi maana kama viongozi tunaweza kusema kupitia vyombo vya habari lakini wanaotazama ni wangapi?”Aliuliza Ridhiwani.
Ametaka kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam, wataalam wa sekta ya ardhi kwa kushirikiana na Meya na viongozi wa mkoa kuwa na kazi ya kufanya katika eneo hilo ili wananchi waweze kujua umuhimi wa kuchukua hati.
Aidha, alisema kamati za urasimishaji makazi holela kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri na manispaa za mkoa kusaidia kuwa sehemu ya uhamasishaji watu kwenda kuchukua hati.
Ridhiwani alisema, kamati za urasimishaji zisiishie katika masuala ya kupanga miji ziende mbali hata baada ya miamala ya malipo inapokuwa imetoka basi wawe sehemu ya kuhamaisha watu waende kulipia ili wapate hati.
Kwa upande wao Makampuni yanayofanya kazi za miradi ya urasimishaji makazi holela walieleza kuwa zoezi hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya wananchi kutolipa pesa kwa wakati tofauti na matarajio kabla ya kuanza zoezi.
Wamesema, zoezi limekuwa na hatua mbalimbali zikiwemo za utambuzi, upimaji na uwekaji mawe na tatizo kubwa lilikuwa katika utekelezaji ambapo lawama kubwa zimeenda kwa makampuni ya urasimishaji na kutolea mfano kuwa kampuni inaweza kuhudumia wananchi 3,000 lakini waliolipa ni 18% pekee na kuongeza kuwa yanapokwenda malalamiko kampuni inadaiwa kula pesa bila kujali asilimia ya kazi iliyofanya.
Kikao kati ya Wizara ya Ardhi na Makampuni ya Urasimishaji Dar es Salaam kimefanyika kufuatia agizo la Waziri wa Ardhi Dkt. Angeline Mabula kuwataka viongozi wa Halmashauri za jiji la Dar es Salaam na Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Mkoa huo kukutana na makampuni hayo ili kukwamua zoezi la urasimishaji.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM