November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mvua yaleta Madhara Sumbawanga

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Sumbawanga

MBUNGE wa Jimbo la Sumbawanga mjini, Aesh Hillary amewaomba wadau wa maendeleo na watu wenye mapenzi mema kuwasaidia baadhi ya wakazi wa kijiji cha Tamasenga ambao wameachwa bila makazi baada ya nyumba zao kubomoka kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Rukwa.

Wito huo ameutoa leo alipokua katika Kijiji hicho akitoa misaada kwa watu ambao wanapitia changamoto kutokana na nyumba zao kubomoka na kupoteza mali mbalimbali ikiwemo vyakula walivyokuwa wamehifadhi kwaajili ya familia zao.

Alisema kuwa baadhi ya wakazi wa Kijiji hicho wanaishi maisha magumu kutokana na nyumba zao kubomoka hivyo wanahitaji misaada ya haraka na nijukumu la wananchi wenzao wenye mapenzi mema pamoja na tasisi mbalimbali kuwasaidia ili nao wapate nafuu ya Maisha.

“watu hawa wanahitaji tuwasaidie, wananchi wenye mapenzi mema, wadau wa maendeleo ninawaomba mjitokeze mguswe na tukio hili muwasaidie, mimi nimetoa magodoro na mablanketi, pia wanahitaji vyakula na nguo, kumbukeni vitabu vitakatifu vinatuhimiza upendo, basi tujitolee kwaajili ya ndugu zetu hawa” alisema Hillary.

Awali mwenyekiti wa Kijiji hicho, Alistide Mwanisenga alimweleza Mbunge Hillary kuwa siku ya Desemba 17 majira ya saa 11 jioni ilianza kunyesha mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali pamoja na radi.

Alisema kuwa mvua hiyo ilisababisha nyumba 43 za wakazi wa Kijiji hicho kubomoka na baadhi ya mali za wakazi hao kuharibika kwa maji huku vitu vingine vikibebwa na maji na watu watatu kujeruhiwa katika tukio hilo.

Baada ya kutoa msaada huo, mmoja wa wakazi wa Kijiji hicho Maria Kapele alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga kwa misaada aliyotoa na kuwaomba watu wengine kuwasaidia kwakua wanapitia katika wakati mgumu kwani baadhi ya wananchi wamepewa hifadhi kwa majirani zao na hawana kitu.