September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto wawili wafariki Dunia kwa kula chakula chenye sumu

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WATOTO wawili wa familia moja wamefariki dunia baada ya kula chakula kinachosadikika kuwa na sumu iliyopelekea wapoteze maisha.

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Richard Abwao amethbitisha kutokea tukio hilo Desemba 12 mwaka huu majira ya saa mbili usiku katika kitongoji cha Sumbigu, kijiji cha Ngukumo, Kata ya Nkiniziwa Wilayani Nzega.

Alitaja waliopoteza maisha kuwa ni Laurencia Nassoro (4) na Sadiki Mustafa (3) .

Alisema walionusurika kifo baada ya kula chakula hicho ni mama mzazi wa watoto hao Janeth Jeremia (48) ambaye amelazwa katika kituo cha afya  Busondo na mtoto Lucia Maplos (8).

Alifafanua kuwa siku ya tukio mama na watoto wake hao walikula chakula cha usiku (ugali na maharage) lakini baada ya muda walianza kuumwa matumbo na hali za watoto zikaanza kuwa mbaya walikimbizwa kituo cha afya Busondo kwa ajili ya matibabu .

Baada ya kupatiwa matibabu hali zao ziliendelea kuwa mbaya na hatimaye kufariki na mama naye alianza kusikia maumivu makali ya tumbo na kukimbizwa kituo cha afya Busondo ambako wamelazwa hadi leo akiendelea na matibabu zaidi .


Abwao alisema wamechukua masalia ya chakula hicho ili kuyapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kubaini sumu hiyo ni ya aina gani na kuongeza  kuwa upelelezi wa kitaalam unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo.


Wakati huo huo mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Shabani Abuu (48) mkazi wa Wilaya ya Urambo Mkoani hapa amejinyonga nyumbani kwake kutokana na migogoro ya kifamilia.

Kamanda alisema tukio hilo limetokea Desemaba 12 mwaka huu majira ya saa 10 alfajiri katika eneo la Majengo Mapya wilayani humo .