Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora imemhukumu kunyongwa hadi kufa Elizabert Paulo na marafiki zake 2 wakazi wa kijiji cha Mwamapuli , Wilaya ya Igunga baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuua mume wake ili arithi mali.
Adhabu  hiyo imetolewa jana na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora Angella Bahati ambaye yupo Wilayani Nzega kuendesha kikao cha kesi za mauaji.
Washitakiwa wengine wawili waliohukumiwa  kunyongwa katika kesi hiyo ya mauaji namba 16/2022 ambao walishiriki kumuua Juma Mdunda  ni Dotto Gibe na Saida Maige Kija.
Awali Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Jeni Mandago akisaidiana na Meritto Ukongoji ulidai kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Oktoba 23, 2021 katika kijiji hicho.
Jopo hilo la Mawakili liliiambia mahakama hiyo kuwa siku hiyo majira ya usiku washitakiwa kwa pamoja walimuua marehemu Juma Mdunda kwa kumkata kata mapanga mgongoni, kichwani na shingoni.
Waliongeza kuwa Elizabert ambaye ni mtalaka wa marehemu alikula njama na hao marafiki zake kutenda kosa hilo ili aweze kurithi mali ikiwemo ng’ombe na mashamba.
Ushahidi unaonesha kuwa siku hiyo Elizabeth akiwa na wenzake walimwomba mwanae mkubwa aitwaye Kamuga Juma kushirikiana kutenda kosa hilo ili waweze kurithi mali lakini kijana huyo alikataa.
Baada ya washitakiwa kutiwa hatiani upande wa Jamhuri uliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa kuzingatia kifungu namba 197 cha Sheria ya  Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwa sababu wamekatisha haki ya kuishi ya mtu mwingine.
Washitakiwa katika shauri hili walikuwa wakitetewa na Mawakili wasomi Fadhili Kingu, Salehe Makenga na Ibrahim Kimwega.
Katika shauri hilo Jamhuri ilikuwa na mashahidi kumi ambao waliweza kutoa maelezo yaliyothibitisha  pasipo shaka tukio hilo la mauaji ya kinyama.
More Stories
‘Ni Wasira ‘Makamu Mwenyekiti CCM Bara
15 mbaroni tuhuma wizi wa shehena ya unga wa sembe
Wacheza rafu Uchaguzi Mkuu ujao waonywa