September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya walimu

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online, Dodoma

MAKAMU wa Rais DKT.Philip Mpango amesema,Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inayo dhamira ya dhati ya kuendelea kuboresha maslahi ya walimu  pamoja na kupata stahiki zao.

Dkt.Mpango ameyasema hayo Disemba 15,2022  wakati akifungua Mkutano  Mkuu wa Chama Cha Walimu Nchini (CWT) uliofanyika jijini Dodoma.

Amesema,lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha watumishi wa umma wakiwemo walimu wanaongeza uwajibikaji na utendaji wenye tija  kwa maslahi mapana kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

“Ndio  maana ndani ya miaka miwili serikali imeweza kupandisha vyeo, kupandisha madaraja na kulipa kwa kiasi kikubwa cha malimbikizo ya mishahara ya walimu ambapo katika kipindi cha maika miwili jumla ya walimu 161,438 wamepandishwa vyeo ,walimu 15,160 wamebadilishiwa vyeo baada ya kujiendeleza kielimu.”amesema Dkt.Mpango

Katika kuhakikisha hayo yanafanikiwa katika utekelezaji  amesema,Serikali imeanzisha mifumo ya kielektroniki kwa maana ya mfumo wa  ukusanyaji madeni yasiyo ya mishahara pamoja na mfumo pamoja wa taarifa za kiutumishi na mishahara ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kushughulikia tatizo la madeni na pia kurahisisha upandishaji wa vyeo  kwa wakati.

Aidha amesema “zoezi la kulipa madeni na kupandishwa vyeo ni endelevu hivyo nawasihi kuwa na uvumilivu na kuiamini serikali yenu kuwa ina nia njema ya kuona kwamba malimbikizo yote ya watumishi yanalipwa kama wanavyostahili na waoastahili kupanda vyeo nao wanapanda.”

Hata hivyo ,pamoja na hatua hizo  Dkt.Mpango amemuagiza Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi ,Vijana ,Ajira na wenye Ulemavu Prof .Joyce Ndalichako kuhakikisha ofisi yake inatoa kipaumbele  cha kushughulikia changamoto za walimu kwa kuanzia na walimu wenye umri wa kukaribia kustaafu.

Akisoma Risala ya walimu,Kaimu Katibu Mkuu wa CWT Japhet Maganga alitumia nafasi hiyo kuipongeza  Serikali kwa kutoa nyongeza ya mshahara kwa watumishi huku akisema imepokelewa kwa heshima na taadhima kwa kuzingatia kuwa takribani kwa muda wa miaka sita Watumishi hawakuwahi kuongezewa mishahara.

Hata hivyo alisema, pamoja na nyongeza hiyo, ukizingatia uhalisia wa gharama za maisha kwa sasa, ongezeko hilo limeshindwa kukidhi mahitaji.

“Chama cha Walimu Tanzania, kwa niaba ya Walimu wa Tanzania, tunaiomba Serikali kuona uwezekano katika bajeti ijayo kutoa nyongeza ya mshahara itakayoendana na gharama halisi ya maisha.

 “Aidha, nyongeza ya mshahara ya kila mwaka  izingatiwe ili kuepuka watumishi kurundikana katika kidato kimoja cha mshahara na hivyo kuwanyima haki wengine kwa kuzingatia umri kazini .

Katika Mkutano huo Dkt.Mpango aliwakilishwa na Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako.