November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi kuelimishwa, kukumbushwa wajibu kwa watoto

Na Judith Ferdinand, Times Majira Online Mwanza

Imeelezwa kuwa suala la malezi kwa watoto wazazi wamelipa kisogo na kujikuta zaidi katika shughuli za uchumi na kusahau wajibu wao,hali inayochangia watoto kukumbana na vitendo vya ukatili na kujifunza vitu ambavyo ni kinyume na maadili.

Hivyo Tanzania Home Economics Organization (TAHEA Mwanza),limeanzishwa na kuzindua jarida la MBELEKO ili kutoa elimu kwa wazazi,walezi na jamii nzima juu ya utoaji wa malezi bora kwa watoto ili waweze kukua vizuri na kuwa raia jarabati.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Miradi ya Elimu -TAHEA Mwanza Peter Matyoko wakati akisoma risala katika uzinduzi huo wa jarida la Mbeleko uliofanyika katika Kituo cha Malezi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mtaa wa Igombe, Kata ya Bugogwa, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Peter ameeleza kuwa,ili kuboresha malezi na kuzalisha watoto wenye manufaa kwa jamii na taifa kwa pamoja wanatakiwa kushirikiana kwani ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha malezi bora kwa watoto.

Jarida la MBELEKO linatumia mifano halisi ya utoaji malezi inayoonekana katika familia na jamii zetu na kujaribu kukosoa,kusisitiza na kuboresha malezi hayo kwa kutumia simulizi ambazo zimetoka kwa watu mbalimbali pia.

limetumia vibonzo katika kuonesha matukio yalijitokeza katika familia na mitaani yanayohusiana na malezi ya watoto ili kufikisha ujumbe.

Pia ameeleza kuwa jarida hilo linatoa fursa kwa wazazi,walezi na jamii nzima kujadili kwa pamoja na kutafakari juu ya malezi ya watoto ya wakati huu ili kuchochea mabadiliko na limezingatia uwepo wa elimu ya malezi.

Aidha ameeleza kuwa malezi na makuzi bora ya mtoto yanaendana na lishe hivyo kupitia jarida hilo lina safi maalumu ya mapishi ya vyakula mbalimbali vya kitanzania kwa ajili ya lishe ya mama mjamzito,anaye nyonyesha,mtoto na familia kwa ujumla.

Akizindua jarida hilo,Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Loata Molel, ameeleza kuwa watoto ni kundi linalohitaji kulindwa,jarida hilo linasaidia upatikanaji wa elimu juu ya malezi ya watoto hivyo wazazi na wote waliopata nakala ya jarida hilo wakasome na kutafsiri kwa vitendo ujumbe uliomo.

Kwani malezi na makuzi ya watoto ni eneo ambalo bado linachangamoto kubwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo elimu ipo chini ya namna bora ya kulea watoto pamoja na vitu vya kujengewa uwezo kwa maana ya majarida na vitabu havipo vya kutosha.

“Kwa sasa kuna changamoto nyingi zinazotokana na kukua kwa sayansi na teknolojia,ambayo imeleta mapinduzi sana katika elimu na changamoto kubwa katika namna bora ya kuwalea watoto wetu,wengi ni mashuhuda kwa sasa hivi watoto wengi wanalelewa zaidi na runinga pamoja na mitandao ya kijamii,kuliko sisi tulivyo lelewa miaka 50 iliopita ambapo tulikuwa tunapata fursa ya kukaa na wazazi na kutusimulia hadithi za mafunzo,”

“Siku hizi watoto wapo kwenye runinga na bahati mbaya wakati mwingine maudhui yanayooneshwa humo hayajachujwa na kufanyiwa usahihi kwamba yapi yana faa na hayafai hivyo wazazi wanatakiwa kuwa makini zaidi ili watoto wasiweze kujifunza vitu ambavyo ni kinyume na maadili pamoja na kutenga muda wa kukaa na watoto wao,”ameeleza Loata.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la TAHEA Mwanza, Mary Kabati kupitia jarida hilo wazazi na walezi watapata muongozo mzuri wa kuwalea watoto wao kwa kufahamu changamoto mbalimbali zinazoweza kuwapata pindi wanapokosa malezi bora.

Mmoja wa wazazi waliohudhuria uzinduzi huo Anamaria Mwenge, ameeleza kuwa kupitia kituo hicho kimesaidia wazazi na walezi kujua namna bora ya kuwatengenezea misingi mizuri watoto hasa wakiwa wadogo kuanzia miaka mitatu.Kwani wazazi wengi walikuwa wakifikiria kuwa mtoto kuanza kumtengenezea misingi ni mpaka pale atakapo anza kujifunza kusoma kwa kushika daftari na kalamu.

“Baadae ya kituo hiki nimebaini kuwa mtoto ana mambo mengi ya kujifunza kabla ya kuanza kushika daftari na kalamu,jarida la MBELEKO naimani litatusaidia na kutukumbusha wazazi wajibu wetu wa na namna bora ya kuwajengea msingi watoto kwani hapa katikati tulikuwa tumejisahau na jukumu la malezi tukiwaachia wadada wa nyumbani,”ameeleza Anamaria.

Hata hivyo Mwwnyekiti wa Mtaa wa Igombe A,Mathias Mkatakona ameeleza kuwa tabia za malezi kwenye kanda yao ya kandokando ya ziwa changamoto ipo ya wazazi kushindwa kuhimili kuwalea watoto na kujikita zaidi katika shughuli za kipato.

Wanacho fanya ni kuhamasisha wazazi kuwajibika katika kuwalea watoto wao kuwa na tabia ya msingi ya mtoto kuanza na kujifunza kipi ili wakue katika misingi imara.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Loata Molel, akikata utepe kuashiria kuzindua hafla ya uzinduzi wa jarida la MBELEKO lililoandaliwa na shirika la TAHEA-Mwanza uliofanyika katika Kituo cha Malezi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mtaa wa Igombe, Kata ya Bugogwa, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Loata Molel, akikata utepe katika jarida la MBELEKO akiashiri kuzindua jarida hilo lililoandaliwa na shirika la TAHEA-Mwanza huku kushoto kwake aliyemsaidia kushika jarida hilo ni Mkurugenzi wa shirika la TAHEA Mwanza, Mary Kabati, uliofanyika katika Kituo cha Malezi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mtaa wa Igombe, Kata ya Bugogwa, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Loata Molel, akionesha jarida la MBELEKO baada ya kulizindua jarida hilo lililoandaliwa na shirika la TAHEA-Mwanza huku kushoto kwake ni Mkurugenzi wa shirika la TAHEA Mwanza, Mary Kabati, uliofanyika katika Kituo cha Malezi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mtaa wa Igombe, Kata ya Bugogwa, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Mratibu wa Miradi ya Elimu -TAHEA Mwanza Peter Matyoko wakati akisoma risala katika uzinduzi huo wa jarida la Mbeleko uliofanyika katika Kituo cha Malezi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mtaa wa Igombe, Kata ya Bugogwa, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza,
Baadhi ya watoto na wazazi waliohudhuria uzinduzi wa jarida la Mbeleko uliofanyika katika Kituo cha Malezi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mtaa wa Igombe, Kata ya Bugogwa, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza,