Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa duniani kote mifumo ya elimu imeendelea kubadilika kutokana na mazingira,mabadiliko hayo katika sekta hiyo hayazuiliki kwa kuwa mambo mapya yanaibuka kila kukicha.
Kwa sababu hiyo taasisi nyingi za elimu duniani zimeendelea kubadili mitahala ya elimu na namna ya ufundishaji ili kwenda na mahitaji halisi.
Kutokana na mabadiliko hayo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango, ameeleza kuwa lazima kuhakikisha elimu inayotolewa vyuoni inaendane na mabadiliko ya teknolojia inayoendelea kwa kasi lakini na vipaumbele vya kitaifa ikiwemo ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na uchumi wa bluu.
Makamu huyo wa Rais,alitoa kauli hiyo katika mahafali ya 41 ya chuo Kikuu Huria Tanzania(OUT),yaliyofanyika katika uwanja wa Furahisha Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, ambapo jumla ya wahitimu 4,124 wamehitimu na kutunukiwa vyeti mbalimbali katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, shahada ya kwanza, Shahada ya Uzamiri na Shahada ya Uzamivu (PhD).
“Wakati tunafanya jitihada ya elimu kupatikana kwa wote lazima tuhakikishe elimu yetu ina ubora stahiki,inatuwezesha kwenye ushindani na kutuletea maendeleo ya taifa,”ameeleza Dkt.Mpango.
Ameeleza kuwa,Tanzania kama ilivyo nchi nyingine hivi sasa imekabiliwa na changamoto mbalimbali katika mifumo yake ya utoaji wa elimu,ambapo elimu iliozoeleka na mifumo yake kwa kiasi kikubwa haiendani na mahitaji halisi ya sasa.
Dkt.Mpango ameeleza kuwa vyuo vilivyopo nchini vinalenga zaidi kumuandaa muhitimu kuajiriwa kuliko kujiajiri,dhana hii inaonekana wazi haikidhi mahitaji kutokana na ukweli kwamba hivi sasa idadi ya wahitimu imekuwa kubwa ukilinganisha na nafasi za ajira katika sekta ya umma na binafsi.
“Kama taifa hatuna budi kujitathimini upya ili tuweze kumudu mabadiliko haya katika sekta ya elimu na kuandaa wahitimu ambao wanakuwa na ushindani kwenye soko la ajira katika sekta zote na hata kimataifa pamoja na uwezo wa kujiajiri,”ameeleza Dkt.Mpango.
Kwa upande wake Mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Rasilimali Watu, ambaye ni Mratibu Mkuu katika Ufuatiliaji na Tathimini wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVETALJA), Dkt. Haji Mnasi ameeleza kuwa atatumia ujuzi aliyoupata kujenga watalaam waliobobea katika elimu na wenye kuweza kujiajiri kupitia elimu zao.
“Kupitia elimu nilioipata ni kuendelea kubadilisha mitazamo na kuondoa dhana ya wanafunzi,kuwa wakihitimu moja kwa moja wataenda kupata ajira,tunatakiwa tuwe na akili nyingi sana,tunapaswa kujiajiri na kutumia elimu tunaweza kuungana na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba tunatoa matarajio ya kujiajiri kwa jamii,”ameeleza Dkt Haji.
Msomi huyo ambaye amewahi kuhudumu kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ileje mkoani Njombe kati ya 2016 hadi 2021 ametaja changamoto alizopitia kupata elimu hiyo kuwa ni kusoma akiwa kazini.
“Ni mtihani sana kusoma huku unaendelea kutumikia Taifa, hii imenijenga na kuniongezea morali ya kutoa maarifa niliyoyapata kuijenga jamii yangu na kuzalisha watalaam zaidi,” amesema Dkt. Haji.
Awali Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Joseph Kuzilwa, ameeleza kuwa mahitaji ya elimu ya masafa ni makubwa na gharama za bando zipo juu.
“Tunaomba serikali ije na sera ya kupunguza gharama za bando hizo ili kutoa nafasi kwa wanachuo kusoma kwa urahisi na gharama ya chini,”ameeleza Profesa Kuzilwa.
Akijibu changamoto ya bando la intaneti, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Adolf Mkenda kukamilisha mchakato wa kukiunganisha Chuo hicho kwenye mkongo wa mawasiliano wa taifa.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi