November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zellothe, Mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa wa Arusha, apata kura 683

Na Queen Lema, TimesMajira Online, Arusha

Zellothe Steven amefanikiwa kutetea nafasi yake ya mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha kwa kupata kura 683 na kuwaacha mbali washindani wake .

Msimamizi wa uchaguzi huo,waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda alimtangaza rasmi Zellothe kuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Arusha na kufuatiwa na Robert Kaseko aliyepata kura 281 huku Edna Kivuyo aliyeambulia kura 12 kati ya wajumbe 970 waliopiga kura hizo

Pinda aliwashukuru wajumbe wa Mkutano huo kwa kutimiza demokrasi yao na kufanya maamuzi waliyoyaamua ya kumchagua Mwenyekiti na kusema kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na haki.

“Uchaguzi sasa umeisha kwa amani na utulifu kilichopo mbele yetu ni kuandaa mikakati ya ushindi mapema mwaka 2025”

Katika hatua nyingine Pinda alikerwa na udanganyifu kwa mmoja ya wajumbe ambaye alinaswa na kura 57 zilizokwisha pigwa kwa ajili ya kumbeba mmoja ya wagombea katika uchaguzi huo

Pinda aliagiza kuchukuliwa hatua kwa mjumbe huyo aliyenaswa na kura hizo ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo ili jambo hilo lisijirudie tena kwani ni kitendo cha aibu ndani ya chana.

Mara baada ya kuchaguliwa na kutangazwa kuwa mshindi Zellothe aliwashukuru wajumbe wa Mkutano huo kwa kumwamini tena kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho na kuwaomba ushirikiano ili kuweza kusukuma gurudumu la chama katika kipindi kijacho.

Alisema siri kubwa ya mafanikio katika Chama ni ushirikiano na imani waliomwonyesha katika kipindi cha uongozi wake wa siku 1,089 alizoongoza kipindi cha nyuma unapaswa kuongezwa mara dufu ili kujenga chama imara kwa maslahi ya Chama.

Aidha Zellothe alisisitiza kuwa hatalipa kisasi kwa wabaya wake nankuwaomba ushirikiano “

Naye Mgombea Robert Kaseko aliyeshika nafasi ya pili aliwashukuru wajumbe kwa kumpa kura nyingi sana kwani kura 281 alizozipata ni kura nyingi sana kwake katika historia ya uongozi wake kwani wajumbe walionyesha kumkubali na kuwataka wana CCM Arusha kumpa ushirikiano Mwenyekiti aliyechaguliwa kwani uchaguzi umeisha sasa kilicho mbele ni kukijenga chama kwa maslahi ya Chama.

Alisema binafsi amempongeza kwa dhati kabisa Komredi Zellothe kwa kuaminiwa na wajumbe wa Mkutano huo kwa kuchaguliwa tena katika kipindi cha 2022/27na amemtakia heri katika uongozi wake mwingine wa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Naye Edna Kivuyo Mgombea Mwanamke wa nafasi hiyo ya Uenyekiti aliwashukuru wajumbe wa Mkutano huo kwa kumpa kura alizopata kwani kwake ni kura nyingi kwa kuwa ni mwanzo wa yeye kuanza harakati za kuwani nafasi mbalimbali za chama.

Kivuyo aliwashukuru Viongozi wa Juu wa chama kwa kurudisha jina lake na kuwa miongoni mwa wagombea nafasi ya uenyekiti na kusema kuwa imani hiyo imempa faraja sana ya yeye kuendelea kukitumikia chama kwa nguvu zote bila ya kusukumwa.

Alisema na kuwataka wana CCM kuwa Uchaguzi umeisha na kuwataka kuvunja makundi na kuwa kitu kimoja kwa kukijenga chama kwani wote ni watoto wa Mama Mmoja haina haja ya kugombea fito kwani wote wanajenga nyumba moja.