Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja, ameagiza kila mkoa kuhakikisha unaanzisha kampeni maalumu yakutengeneza mazingira ya ukijani kwa kuweka mikakati madhubuti ya kurejesha uoto wa asili nchini.
Naibu Waziri huyo anasema tayari kampeni hiyo inafanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS katika mkoa wa Dodoma na kuonyesha mafanikio makubwa kwa kujulikana kama Dodoma ya kijani na kwamba sasa imefika wakati ianze kufanyika katika mikoa yote nchini.
Mhe. Masanja alitoa kauli hiyo jana Novembe 22, 2022 mkoani Dar es Salaam wakati akizindua warsha ya urejeshaji wa uoto wa asili (AFR100) iliyowakutanisha wadau mbalimbali wanaotekeleza shughuli za uhifadhi nchini lengo likiwa ni kujenga msingi wa kuandaa taarifa za pamoja ya nchi ya utekelezaji wa makubaliano ya nchi kurejesha uoto wa asili iliyoyafanya mwaka 2018.
Tanzania ni Miongoni mwa nchi ambazo zinashirikiana na Dunia kuhifadhi misitu yake ambapo hadi kufikia mwaka 2030 inatakiwa iwe imerejesha uoto wa asili katika eneo la hekta milioni 5.2 na kwamba ili kufikia huko, kuna haja ya kila mkoa kuanzisha kampeni hiyo ya kuwa na ukijani wake ambayo itatokana na kuweka mikakati madhubuti ya kutunza mazingira na kurejesha uoto wa asili. .
“Tanzania ni miongoni mwa nchi 54 zilizoingia kwenye mkataba wa urejeshaji wa uoto wa asili ambao kati ya hizo, tayari nchi 32 zimesaini mkataba na kuingia katika utekelezaji wa uoto huo,”alisema Masanja.
“Malengo ya dunia ni kuhakikisha kwamba jumla ya hekta milioni 350 zinarudi kwenye uoto wa asili, kwa Afrika tuna malengo ya jumla ya hekta milioni 100 ambazo zinatakiwa kurejeshwa kwenye uoto wa asili. Tanzania tumejiwekea malengo ya kurejesha uoto huo wa asili kwa hekta milioni 5.2 mpaka kufikia mwaka 2030.”
“Kwa hiyo serikali katika kufanikisha lengo hilo, iliamua kuhusisha wadau mbalimbali ikiwamo kutoa elimu ili waingia kenye mpango huo. Na baada ya kuingia tulibaini kwamba kuna maeneo ambayo tayari yamekwishakuvamiwa na wananchi ambayo kiukweli yalistahili kuhifadhiwa vizuri.”
Kamisha wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo anasema katika kufanikisha hilo la kurejesha uoto wa asili wanahakikisha kwamba maaeneo ya misitu yaliopo nchi kavu na baharini sambamba na maeneo ambayo yana mito na uoto wa misitu hayaharibiwi.
“Na hata yale ambayo yameharibika kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu, iwe ni uvamizi kwa ajili ya makazi, shughuli za uvunaji wa nishati ya mkaa na nyinginezo, kuhakikisha yanarejesha uoto wake wa asili kwa kupanda miti katika maeneo yote ambayo yameharibika na hata katika maeneo mengine ambayo hayajaharibiwa ili kutoa mbadala wa mazao ya misitu katika maeneo hayo,” anasema Prof. Silayo.
“Katika kufanikisha hili, wadau mbalimbali wanatakiwa kushiriki ikiwamo wananchi, serikali, mashirika na asasi za kiraia. Na mkakati huu unalenga siyo kuboresha mazingira yaliyoathirika, lakini kuhakikisha kwamba jamii zinazoishi katika maeneo mbalimbali zinanyanyuliwa kiuchumi.”
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti