November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu wapatiwa mafunzo elimu Jumuishi

Na Esther Macha, Timesmajira, Online, Mbeya

WALIMU wanaofundisha watoto wenye ulemavu kutoka Mikoa ya Mbeya, Rukwa na Dodoma wamepatiwa mafunzo maalum ya elimu jumuishi ili waweze kuwalea na kuwasaidia watoto katika ulinzi Jumuishi.

Edward Majura ni Mratibu wa miradi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Child support Tanzania (CST)amesema hayo leo wakati wa mafunzo kwa walimu wanaofundisha watoto wenye ulemavu kwa baadhi ya Mikoa.

‘Mara nyingi watoto wenye ulemavu wanakuwa katika hatari kwa mujibu wa takwimu za UNICEF zinasema kuwa watoto wenye ulemavu wapo mara nne ya kufanyiwa vitendo vya kuvunja haki zao hivyo ni vema tukawapa maarifa namna gani walimu wanaweza kushiriki kumlinda mtoto na kumtetea”amesema.

Walimu kutoka mikoa mitatu nchini wakiwa katika mafunzo mkoani Mbeya.

Aidha Majura ameeleza kuwa pamoja na hayo pia walimu watapewa maarifa juu ya kufundisha elimu Jumuishi na namna gani darasa lenye watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu jinsi wa navyo wenza kufundishwa kwa wakati mmoja.

Akifafanua zaidi Majura amesema kuwa wanashikiliana na watalaam kutoka Child support Tanzania na Chuo Kikuu cha AMUCTA ambapo kwa pamoja watatoa elimu na mbinu ambazo wanaweza kuzitumia, kubaini uwezo kwa wanafunzi namna ya kujifunza.

Hata hivyo amesema kwamba Child support Tanzania inatekeleza mradi ambao upo chini ya ubarozi wa Ujerumani na kuwa mradi huo una lengo kuu la kutengeneza mazingira Jumuishi na salama kwa watoto wenye ulemavu nchiniTanzania.

Amesema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha watoto wote wenye ualubino na uoni hafifu na udumavu wa kuona wanasajiliwa na kuanza shule.

Akielezea zaidi Mratibu huyo amesema kuwa moja ya shughuli zake ni kufanya mafunzo kwa walimu ambapo walimu wake ni kutoka Hoboro, Bwigiri zilizopo Mkoani Dodoma nyingine ni Katumba, Child support, ambazo zote zipo mkoani hapa.

Fraterinus Mutatembwa ni Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha AMUCTA kilichopo mkoani Tabora amesema kuwa changamoto iliyopo kwa jamii kwa watoto wenye ulemavu ni kuwa jamii inaweka changamoto kwa watoto wenye ulemavu kushindwa kujifunza vizuri na kusema kuwa ili watoto wenye ulemavu kujifunza lazima jamii Ibadilike pamoja na kutengeneza mazingira rafiki kwao ili waweze kupata elimu stahiki.

Hildergade Mehrab ni Meneja Miradi wa Taasisi ya Child Support Tanzania amesema kuwa mafunzo hayo kwa walimu yanajumuisha walimu 24 kutoka mikoa ya Mbeya, Rujewa, Dodoma.

Aidha Mehrab amesema kuwa wamejikita kwenye elimu Jumuishi kuanzia aina za ulemavu unaooneka na usiooneka jinsi ya kuwatambua kufanya tathimin.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Katumba iliyopo Wilayani Rungwe amesema kuwa mafunzo waliyopatiwa yatasawasaidia namna ya kulea watoto katika njia bora zaidi, uboreshaji wa miundombinu ya shule ya kujifunzia na kufundishia watoto.