November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yasimamisha uchaguzi baadhi ya mikoa nchini

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesimamisha uchaguzi katika mikoa mitatu kwa nafasi zilizoonyesha kuwa na changamoto pamoja na kufuta uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM kwa sababu ya rushwa.

Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo kwa dhamana ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa uchaguzi wa ndani ya chama unaoendelea ambao umefikia ngazi za mikoa chama na jumuiya,ametangaza kufuta uchaguzi katika baadhi ya maeneo na kusimamisha mchakato wa uchaguzi na kutuma timu za uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Novemba 21 2022,Chongolo amesema baada ya tukijiridhisha kama hakutakuwa na changamoto chama kitaruhusu  uchaguzi kufanyika na kama watabaini  changamoto wataondosha wagombea wenye changamoto na wasio na changamoto kuendelea na uchaguzi kwa nafasi husika.

Aidha chama hicho kimesema, baada ya uchunguzi wa kina wa changamoto katika maeneo husika ,hatua zaidi zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wahusika kugombea na kisha kuwakabidhi katika vyombo vyenye dhamana ya kufuatilia masuala ya rushwa.

“Mikoa ambayo tumefanya  uamuzi ni pamoja na kufuta uchaguzi wa umoja wa Vijana mkoa wa Simiyu , pia tumesimamisha uchaguzi wa mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mbeya kwa sababu ya tuhuma mbalimbali zikiwemo za rushwa ambako nako tunafanya uchunguzi wa kina tukikamilisha tutatoa taarifa ya uamuzi wa chama,

“Vile vile tumesimamisha uchaguzi wa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM  mkoa wa Arusha kwasababu hiyo hiyo ya rushwa na  tukikamilisha uchunguzi tutatoa taarifa za uamuzi wa chama ili kuruhusu mchakato wa uchaguzi kuendelea,”amesema Chongolo

Wakati huo huo Chongolo amezungumzia kuhusu tukio la wanachama kuondoka na boksi la kura katika uchaguzi uliofanywa jana mkoa wa kichama wa Magharibi Zanzibar amesema kuwa taarifa zilieleza kuwa watu hao walienda na boksi hilo kwenye chumba kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya kuhesabia kura .

“Sasa tunataka kuangalia uchukuaji wa boksi hilo ulilenga kuhesabu kura au ulikuwa una lengo lingine,tutafuatilia tukijiridhisha tutachukua uamuzi ukiwemo kuufuta uchaguzi na kurudiwa upya ili kutenda haki ,tukijiridhsihsa kwamba lengo la  kuchukua boksi hilo ulilenga kwenda  kuhesabu kura basi tutaruhusu matokeo ya uchaguzi huo yaendelee kama yalivyo,”amesema

Pamoja na hayo Chongolo amezungumzia kuhusu changamoto iliyopo sasa ndani ya chama hicho kuwa ni kuwepo kwa wajanja  wachache wanaogombea nafasi mbalimbali au wapambe wao kutengeneza msukumo wa kuonyesha wao ni maalum kuliko wengine  na wao ndio wanaotakiwa na viongozi wa juu kuliko wengine.

“Wapo humu wengine wanajiita wagombea wa katibu Mkuu ,wapo wanaojiita wagombea wa Makamu Mwenyekiti ,wengine wanajiita wagombea wa Mwenyekiti na wapo wanaojiita wagomeba wa wajumbe wa kamati kuu,

“Sisi tulishapitisha majina,na  kama tumepitisha kwenye mkoa majina matatu ,moja ,mawili au manne na kuendelea maana yake hao ndiyo wagombea wa chama,mtu yeyote anayetumia hila na ujanja ujanja wa kutengeneza maneno kwamba yeye ni mgombea wa mtu anaonyesha ni namna gani anatakiwa kuwasaidia wapiga kura kuamua na siyo kutengeneza  uongo maana hakuna kiongozi ambaye ana mgombea ,

“Ndiyo  maana hujaona Katibu Mkuu akienda mkoa wowote kwenda kumpigia debe mgombea hii ni kwa sababu wagombea tuliowapitisha kwenye vikao vyetu ndiyo wagombea wa chama,kwa hiyo tuache ujana wa kutumia majina ya viongozi, tuseme sera na tuonyeshe uwezo wetu ,na kama tumewafanyia mazuri wanachama tutakubalika lakini tuwaache wajumbe wachague mtu wanayemuona kuwa ni sahihi badala ya kutumia hila ,ujanja ujanja , uzushi kusingizia na maneno mengine kama hayo,”amesema Chongolo.