Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni changamoto kubwa ulimwenguni hali ambayo imechangia ukame pamoja na kuwa na mvua zisizotosheleza.
Huku hali hiyo ya mabadiliko ya tabianchi yakichangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo uchomaji na ukataji wa miti bila kuzingatia kanuni ya kupanda miti kabla ya kukata miti pamoja na uchafuzi wa mazingira ikiwemo utupaji wa taka ovyo.
Kufuatia changamoto hiyo Serikali imekuwa ikisisitiza kila mwananchi kufuata ajenda ya utunzaji wa mazingira na upandaji miti ili kufikia lengo la kupanda miti millioni 276 kwa mwaka ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Wilaya ya Ilemela ni miongoni mwa Wilaya zilizopo nchini hapa,ambayo imechukua hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuunga mkono jitihada za serikali za upandaji wa miti.
Ambapo Wilaya ya Ilemela imepanda miti 200 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi nchini.
Katibu Tawala Ilemela,ahamasisha jamii juu ya upandaji miti
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la upandaji miti katika shule ya msingi Buswelu Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Said Kitinga kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, ameeleza kuwa upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira ni jambo linalohusu maisha ya binadamu wote.
Hivyo jamii ya Ilemela inapaswa kupanda miti pamoja na kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira.
“Jambo hili linahusu maisha yetu kwa ujumla wake pamoja na kizazi kilichopo na kinachokuja,tusipoweka mazingira yetu vizuri bado tunahatarisha maisha yetu,”ameeleza Kitinga.
Wito kwa viongozi wa dini
Mbali na hayo Kitinga ametoa wito kwa viongozi wa dini waliopo wilayani humo kuwa mstari wa mbele katika kuwahubiria waumini wao habari za upandaji miti na utunzaji wa mazingira kwa ujumla wake.
“Utunzaji wa mazingira unahusu jamii nzima,sehemu sahihi ya kupeleka elimu hii ya mazingira ni kwa waumini wa dini zote, waambiwe ukweli kwamba uharibifu wa mazingira ni dhambi kwani unaathiri uhai wa binadamu na viumbe hai vilivyopo,”ameeleza Kitinga.
Huku Kamati ya Amani Wilaya ya Ilemela kuwajibika katika masula ya utunzaji wa mazingira na kuandaa kampeni za ushawishi kwa kutambua kuwa mazingira salama ndio uhai wa watu wote.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) yaeleza umuhimu wa upandaji miti
Mwakilishi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Tito Mwasumbi, ameeleza kuwa wanaunga mkono juhudi za Rais na kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais,juu ya upandaji miti isiyopungua 1,500,000 kila Halmashauri nchi nzima.
Ameeleza kuwa kufuatia zoezi la upandaji miti shuleni hapo nyumba zilizopo jirani na shule hiyo ya Buswelu zitanufaika na uwepo wa miti pindi upepo unapokuwa mkali kwa kuwa miti inapunguza kasi ya uharibifu wa mazingira.
“Miti uzalisha hewa nzuri na kuleta mazingira ya kuvutia ni wajibu wa jamii hii kuhakikisha miti yote inakuwa kwa viwango vinavyokubalika,”ameeleza Mwasumbi.
Mwanafunzi na Mwalimu shule ya msingi Buswelu wazungumza zoezi la upandaji miti
Mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Buswelu Justin Winfred, ameeleza kuwa faida za miti ni pamoja na uwepo wa hewa safi ya oksijeni,vivuli wakati wa jua,mazingira yenye mvuto,mazao ya miti kama matunda na mbao.
Mwalimu wa Mazingira shule ya msingi Buswelu Mariam Samson,amehimiza jamii zilizopo jirani na maeneo ya shule hiyo kuunga mkono juhudi hizo kwa kulinda miti hiyo isiibiwe wala kuharibiwa na mifugo.
Kiongozi wa dini anena juu ya upandaji miti
Mchungaji Kiongozi wa kanisa la Highway of Holiness Church (HCC) Buswelu,
Elisha Msanifu, ameeleza kuwa kanisa hilo lina mpango wa kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuboresha mazingira ya taifa hili.
Mchungaji Elisha, ameeleza kuwa kama kanisa wanaandaa kampeni ya utunzaji wa mazingira ambayo itahusisha masuala ya upandaji miti hivyo wakiwa tayari watatoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya Wilaya.
Balozi wa Mazingira.
Kwa upande wake Balozi wa Mazingira Mrisho Mabanzo maarufu kama “Mr Tree” ameihamasisha jamii kupanda miti na kutunza mazingira kupitia kauli mbiu isemayo “Tanzania Yangu, Mazingira Yangu Nayapenda Daima”
Katika zoezi hilo jumla ya miti 200 imepandwa ambayo ilitolewa na TFS likiongozwa na Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela Said Kitinga kwa kushirikiana na Balozi wa Mazingira Mrisho Mabanzo maarufu kwa jina la “Mr.Tree” kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania katika kampeni ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti