November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

FAO, MPC wajadili usalama na upotevu wa chakula, wakiangazia sekta ya uvuvi

Na Daud Magesa na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) imekutana na ujumbe kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na kufanya mazungumzo mafupi ya upotevu na usalama wa chakula.

Mazungumzo hayo yaliofanyika jana katika ofisi za MPC yalielenga kufanya kazi pamoja katika eneo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari na wanachama wa MPC kuhusu usalama,uhaba na upotevu wa chakula pamoja na mazao ya uvuvi (Food loss and West Assessment).

Katika mazungumzo hayo FAO iliongozwa na Omar Riego Penarubia na Dr. Julia Heye ambapo MPC iliwakilishwa na Mwenyekiti Edwin Soko,Mjumbe wa Bodi ya UTPC,Jimmy Luhende na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa Omar Penarubia FAO inafanya mradi wa utafiti katika nchi tatu za Colombia (Marekani), Sri Lanka (Asia) na Tanzania barani Afrika ili kufahamu ukubwa wa changamoto hiyo ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na namna ya kuikabili.

Pia utafiti huo wa kiuchumi na kijamii unalenga kufahamu nani wako kwenye mnyororo wa thamani katika mazao ya samaki,mdau yupi atafanya nini, uwezeshaji wanawake ili kuwafanya wawe na uwezo na uelewa katika uzalishaji chakula na upotevu wa chakula hasa vijijini.

“Tunataka kuwa na takwimu sahihi ni kwa kiwango gani cha rasilimali za uvuvi (samaki hasa dagaa) na chakula kinapotea wakati wa mavuno,utunzaji na usafirishaji hadi sokoni,jinsia,miundombinu,sheria na kanuni,”alisema Omar.

Alisema waandishi wa habari watajengewa uwezo wa matumizi ya teknolojia ya kisasa wanapotekeleza majukumu yao yakiwemo masuala mengine ya kiuchumi na kijamii, pia waandishi habari watatumia jarida la FAO linalochapisha habari na makala mbalimbali zinazohusu chakula.

“Vyombo vya habari ni muhimu katika ushirikiano sawa na umuhimu wa shirika hilo kusaidia kundi la waandishi wa kutumia teknolojia kutekeleza majukumu yao,”alisema Omar.

Kwa upande wake,Soko alisema MPC iko tayari kushirikiana na FAO katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ukiwemo uwezeshaji wa mafunzo ya kitaaluma kwa wana habari ili kuwafanya wawe weledi katika masuala ya usalama,uzalishaji na upotevu wa chakula.

Wawakilishi kutoka FAO Omar Riego Penarubia( kushoto) na Dr. Julia Heye(kulia) walipotembelea KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) na kufanya mazungumzo mafupi ya upotevu na usalama wa chakula.