Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online Mwanza
Imeelezwa kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ina mtandao wa barabara wa Kilomita 875.75.
Ambapo kati ya kilomita hizo barabara za lami ni km 35.26, zege km 1.52, mawe km 2.07, changarawe km 60.18 na udongo km 776.83.
Hivyo ili barabara hizo ziweze kudumu Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela limekutana na TARURA Wilaya ya Ilemela kwa ajili ya kujadili mustakabali wa barabara zinazopatikana katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho Msahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga,ameishauri TARURA kutengeneza barabara za mawe na mitaro imara kutokana na halmashauri hiyo kuwa na Kata nyingi zilizopo kwenye mwinuko.
Hii itasaidua kudumu na thamani ya fedha ionekane huku akihimiza usimamizi mzuri na juhudi katika matengenezo ya barabara hizo.
Sanjari na hayo Mulunga,amesisitiza kuwa Mkurugenzi na wataalam wote kuhakikisha wanatilia mkazo suala la ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha upatikanaji wa bilioni 1.2 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.
“Fedha hiyo itatolewa katika Kata zote kwa uwiano sawa,tumepitisha kwa kauli moja kuwa kupitia fedha hizo za mapato ya ndani kila Kata itapata milioni 63 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na hivyo Madiwani ainisheni barabara chache ili zitengenezwe katika ubora na thamani ya fedha iweze kuonekana,”amesisitiza Mulunga.
Baadhi ya Madiwani wakiwasilisha hoja zao juu ya barabara zinazopatikana katika kata zao kwa nyakati tofauti,wameitaka TARURA kuhakikisha kuwa barabara zote za halmashauri hiyo,zinawekwa katika mpango wa matengenezo na zinatengenezwa kwa kiwango cha mawe au zege ili ziweze kudumu.
Pamoja kutengeneza mitaro na makalavati imara ili kuwezesha barabara hizo kudumu na zisiharibiwe na mvua zinazoendelea na kukamilisha barabara hizo kwa wakati ili zipitike nyakati zote.
Huku kwa upande wa barabara ambazo zinaelekea katika taasisi mbalimbali kama shule hospitali na zingine kuhakikisha zinapewa kipaumbele kwani sehemu ambazo wananchi wanaenda kupata huduma za kijamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary ameeleza kuwa Ilemela imetenga kiasi cha bilioni 1.2 itakayotoka katika mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya matengenezo ya barabara ikiwa ni maelekezo ya Serikali Kuu ya kuzitaka halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya barabara.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa matengenezo ya barabara Wilaya ya Ilemela,Meneja TARURA Wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo, ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya mikataba 9 ya utengenezaji wa barabara inatarajiwa kutekelezwa na hadi sasa wameisha ingia mikataba 7.
Ambapo kati ya miradi hiyo miradi miwili imekamilika, miradi 5 inaendelea na miradi miwili ipo hatua ya manunuzi.
Ameeleza kuwa TARURA Wilaya ya Ilemela imetenga kiasi cha bilioni 2.6 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ambapo bilioni 1.6 ni kutoka Bodi ya Barabara,milioni 500 za mfuko wa Jimbo na bilioni 1 ni fedha za tozo za mafuta na kuongeza kuwa hadi sasa fedha iliyoidhinishwa ni kiasi cha milioni 500.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi