Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Kilindi
MKUU wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba amewapa siku 14 Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi wawe wamemaliza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo.
Ni baada ujenzi huo kuchelewa kukamilika kwa muda uliopangwa kwa majengo ya awali, huku sababu zikitolewa kuwa ni kuchelewa kupokea fedha za ujenzi kutoka kwenye mfumo, lakini pia ni gharama za uendeshaji, ambapo Mgumba hakukubaliana na sababu hizo.
Alitoa maagizo hayo Oktoba 29, 2022 alipotembelea, na kukagua ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa Kata ya Bokwa, kwenye viunga vya Mji wa Songe yalipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi.
Mgumba alisema, kutokana na maelezo yaliyopo kwenye nyaraka, inaonesha ujenzi wa Awamu ya Kwanza ambao ni jengo la Wagonjwa wa Dharura (EMD), Wagonjwa wa Nje (OPD), maabara na nyumba ya watumishi wa afya yenye uwezo wa kuishi kaya tatu (three in one), ulikuwa uanze Januari hadi Aprili, mwaka huu.
Lakini kutokana na changamoto mbalimbali, ujenzi huo ukashindwa kukamilika muda huo, na kuongeza muda mwingine hadi Juni 30, mwaka huu, lakini pia bado ujenzi huo ulishindwa kukamilika hadi sasa, ambapo ujenzi huo kwa majengo ya hospitali umefikia asilimia 65, huku ujenzi wa nyumba ya watumishi ukifikia asilimia 98.
“Natoa siku 14 ujenzi wa majengo haya ya hospitali yawe yamekamilika. Mimi naamini mngefuata muongozo, na maagizo ya viongozi wa juu, ujenzi huu wa hospitali ungekuwa umekamilika, lakini badala ya kufuata muongozo huo, mliamua kuongeza ujenzi wa majengo mengine bila utaratibu na kujikuta mnakwamisha ukamilishaji wa hospitali.”
“Halafu mnaposema gharama za vifaa imepanda mimi nakataa sababu, Kata ya Bokwa kwa kutumia sh. milioni 60 imejenga vyumba vipya vya madarasa vya sekondari vitatu, na kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari vitatu. Ina maana kwenye kata mfumo ulifunguka, lakini halmashauri haukufunguka. Au vitu vilipanda bei kwenye halmashauri, lakini kwenye kata vilishuka” alisema Mgumba.
Mgumba alisema Serikali ilitoa sh. milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa awali wa hospitali ikihusisha jengo la OPD na maabara. Pia ikatoa sh. milioni 300 kwa ajili ya jengo la Wagonjwa wa Dharura, huku ikitoa sh. milioni 90 kujenga nyumba yenye uwezo wa kuishi watumishi watatu.
“Pamoja na kuchelewa kukamilisha hospitali hii, lakini lazima niwapongeze. Ujenzi wa majengo yenu ni wa viwango vya juu” alisema Mgumba.
Baadhi ya wataalamu walimueleza Mgumba kuwa kutokana na hospitali hiyo kuwa mpya, baadhi ya wataalamu wa afya walishauri kujengwe jengo la wodi ya akina mama, na ndani yake kuwe na chumba cha huduma ya upasuaji.
Maamuzi hayo ndiyo yamefanya kushindwa kukamilisha majengo yaliyokusudiwa kwa wakati, na kufanya hadi sasa ujenzi wake kufikia asilimia 65, huku fedha iliyobaki kwa ajili kazi hiyo ikiwa ni sh. milioni 72.Huku Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Kahindi Mathusela akieleza sababu nyingine iliyofanya mradi huo kuchelewa kuanza.
“Mradi wa Hospitali ya Wilaya, fedha zimefunguliwa kutumika mwezi wa tano mwaka huu. Hata hivyo, vifungu vya matumizi baada ya mwaka wa fedha kuisha, vimechelewa kufunguka” alisema Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Kahindi Mathusela.
Akizungumza na uongozi wa Wilaya ya Kilindi ikiwemo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye kikao kilichofanyika Ukumbi wa Halmashauri hiyo, alituma salamu kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara, Vitengo, watendaji na watumishi wa umma kuwa, kuanzia sasa, ziara zake zitakuwa ni kukagua miradi, na sio kuona miradi. Atataka kila mradi uoneshe viambatanisho vyake.”
Kuanzia sasa sitafanya ziara kutembelea miradi, bali nitafanya ziara hizo kukagua miradi. Nataka miradi nitakayotembelea nikute nyaraka zote zinazoonesha mradi huo utaanza lini na kumalizika lini. Umetumia kiasi gani cha fedha, na utatumia kiasi gani hadi kukamilika kwake. Nataka salamu hizi ziwafikie Wakurugenzi wote wa Mkoa wa Tanga” alisema Mgumba.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito