Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe na kutoa wito kwa Wakurugenzi wa Wizara ya Afya kuwa na uwajibikaji wenye tija kwa wakati.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Jijini Dodoma ambapo baada ya kukabidhiwa ofisi Prof. Nagu amezungumza na Wakurugezi wa wizara na kuwataka kutumia Rasilimali zilizopo vizuri kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha agenda ya afya kwa watanzania inakuwa imara.
Akizungumza Prof. Nagu amesema kuwa wakurugenzi hao watumie utaalamu, uadilifu,uwajibikaji wa kiwango cha juu na haraka sana katika kuwahudumia watanzania kuwa na afya bora.
Kwa upande wake aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini katika kipindi alichokuwa katika nafasi hiyo.
“Niwaombe wakurugenzi wote mpeni ushirikiano Prof. Nagu na endelezeni yale mazuri yote tulokuwa tunafanya katika kuwatumikia watanzania”, ametoa rai Dkt. Sichalwe
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa Wizara ya Afya, Dkt. Elias Kwesi ametoa shukrani kwa niaba ya wakurugenzi wote na kusema wataendeleza mazuri yote waliyopata kutoka kwa Dkt. Sichalwe.
Dkt. Kwesi amesema wapo tayari kuwajibika kwa kutoa ushirikiano wa karibu kwa Prof. Nagu ili kuleta tija katika kuimarisha agenda ya afya nchini.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba