Na Penina Malundo, Timesmajira,Online
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewaonya wote wenye dhamana ya kusimamia mali za Chama wafanye kwa uadilifu kwani hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kupoteza nyaraka za mali hizo.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam leo wakati akiweka jiwe la msingi ya ujenzi wa ofisi CCM wilaya na nyumba ya Katibu Mkuu wa Chama mkoa wa Dar es Salaam zilizopo wilayani Kigamboni.
Amesema mwaka 2017-2018, Chama kilifanya kazi ya kutambua mali na rasilimali zake na kutengeneza orodha ndefu na kuwekwa mpango wa kuzisajili ambao ulikamilika.Chongolo amesema baada ya usajili kukamilika Chama kiliamua kutengeneza utaratibu wa kuzimiliki mali hizo kisheria.
“Jambo linalosikitisha ni kasi katika maeneo mbalimbali ya kuendelea kutafuta nyaraka za umiliki kisheria wa maeneo imepungua na baadhi wameanza kuacha na kuona sio sehemu ya majukumu yao,” amesisiitiza.
Aidha amesema moja ya kigezo watakachompima mtendaji wa Chama katika ngazi yotote ni namna anavyoshiriki katika kila eneo ambalo limeandikwa kuwa sehemu ya wajibu wake na siyo vinginevyo.
“Inasikitisha kuona mali tulizomiliki kwa karne, kwa miaka mingi, leo mtu anajitokeza na kusema hapa kwangu na sio ajabu kwa kutamka hivyo anapata fursa ya kusumbua na hata kutengeneza mazingira na kujitengenezea uhalali, wakati wenye mali ambao ni Chama ngazi husika wapo na wanayaona hayo wamekaa kimya na wanasubiri miujiza, hili hatutalikubali,” amesema.
Chongolo amewahakikishia wana CCM kuwa litakapotokea tukio la namna hiyo hatua kali zitachukuliwa kwa mtendaji aliyepo katika ngazi husika na kwenye hilo hatakuwa na mzaha.
Akizungumzia Chaguzi ndani ya CCM amesema Chama hicho bado kinakabiliwa na changamoto ya rushwa katika ngazi ya wilaya kwani walibaini baadhi ya watu kufanya rafu za kikiuka taratibu za uchaguzi na kufuta matokeo ya wilaya 21 na uchaguzi kurudiwa.
“CCM ina bahati ya kuwa na wanachama wengi, wazuri, wenye uwezo mzuri wa kiakili, kiuongozi na wenye moyo na mapenzi mema na dhati kwa Chama,”amesema
More Stories
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta