November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Katanga akitaka chama cha wahandisi ACET kutoa mafunzo

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga amekitaka Chama cha Wahandisi Elekezi nchini (ACET) kutoa mafunzo na usimamizi makini kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa nchili kuimarisha miundombinu na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Akifungua mkutano wa 36 wa ACET katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu wizara ya ujenzi na uchukuzi(sekta ya ujenzi), Ludovick Nduhiye amesema pamoja na changamoto mbali mbali serikali imeanza kuamini miradi inayotekelezwa na wakandarasi wazawa.

Aliwataka kuhakikisha wanakuwa na dhamira ya dhati, utayari na ufanisi wa hali ya juu katika utekelezaji wa miradi na kusisitiza kuzingatia maadili pindi wanapopata fursa ili kujenga imani.

“Serikali itaendelea kuwashirikisha katika miradi ya ndani ya kimkakati lakini lazima mzingatie ubora wa miradi inayotekelezwa ili iendendani na thamani ya fedha iliyowekezwa” alisema Balozi Katanga.

Alisema utekelezaji wa miradi wanayopewa uzingatie tija, ufanisi na wafuate maadili ili kudhibiti vitendo vinavyoweza kusababisha miradi kuwa na viwango hafifu na kutokuwa na thamani halisi ya fedha iliyowekezwa.

Balozi Katanga aliwataka kujiepusha na utoaji na upokeaji wa rushwa kwani kwa kiwango kikubwa unachangia katika viwango duni katika miradi ua ujenzi wa miundombinu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi.

Awali Rais wa ACET, Deo Mugishwage aliiomba serikali kuendelea kuwajengea uwezo wahandishi elekezi ili waweze kuhimili ushindani dhidi ya makampuni ya kigeni .

Alisema ACET imebaini moja ya sababu kubwa ya kukosa kazi ni biashara ya uhandisi ushauri na elekezi imehodhiwa na makampuni ya nje huku makampuni ya kizalendo yakikabilliwa na changamoto ya mtaji mdogo hivyo kushindwa kuhimili ushindani katika mashindano ya zabuni.

Mwenyekiti wa mkutano huo, Ngwisa Mpembe alisema mkutano huo unawapa fursa ya kubadilishana uwezo na kuwapa serikali mrejesho wa changamoto wanazozipata kwenye usimamizi na utekelezaji wa miradi.

Aliishukuru serikali kwa kuwapa kazi za ushauri elekezi na ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo wahandisi wazalendo ili kuboresha uwezo waoKwa upande wake , Farida Mawenya aliwataka wahandisi elekezi wanawake kujitokeza na kuchangamkia fursa na kutatua changmoto zinazowakabili.

Farida ambaye ni mwekahazina wa ACET amesema mwaka huu wamejipanga kutekeleza mraji wa kuwajengea wanawake wahandisi elekezi katika uongozi .