November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Angeline: Jamii kuweni wa wazi zoezi la sensa kwa kutoa taarifa ikiwemo za watu wenye ulemavu

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Rai imetolewa kwa jamii kuwa wa wazi katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agousti 23,2022 kwa kutoa taarifa za watu wote hata kama ni mtu mwenye ulemavu,ili kufanikisha mipango ya serikali katika kuwaleta wananchi huduma.

Hiyo ni kutokana na kuwepo kwa tabia ya baadhi ya watu kuwaficha watu wenye ulemavu ili wasihesabiwe.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,wakati akizungumza na wanawake wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikiwa ni kundi la tatu ambao wamepata mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022, na mapambano dhidi ya ukatili yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani hapa.

Dkt.Angeline, ameeleza kuwa Serikali imezungumza kuwa watu wanatakiwa wawe wa wazi katika zoezi la sensa ya watu na makazi hata kama mtu anayeishi na mtu mwenye ulemavu atakuwa amemficha basi jirani yake anayejua atoe siri au taarifa ili iweze kujua.

“Ni kweli wapo wanaoficha serikali inaendelea kila siku kuzungumza suala hilo kwaio Mimi nitoe Rai kwa watanzania tunapoishi katika jamii zetu tunafahamiana huyu yupo na nani ana watoto wangapi kama ana mtoto mlemavu tunajua hata kama anamficha pengine ulikwisha sikia kuwa ana mlemavu ni kutoa taarifa kwa serikali ili angalau watoto waweze kufikiwa,”ameeleza Dkt Angelene.

Pia ameeleza kuwa lengo la serikali ni asiachwe mtu nyuma kwani inapokwenda kupanga mipango yake lazima iwe imehusisha makundi yote na iwe na uhakika na takwimu zake bila hivyo maana yake mipango yake haitakuwa sahihi itapanga mipango kwa watu milioni 50 kumbe wameishafika watu milioni 55.

“Maana yake wale waliozidi watakuwa wanafaidi mipango ya watu wengine ambao wamewekewa kwa ajili ya maendeleo yao matokeo yake tunakuwa na upungufu wa hapa na pale kwenye huduma za jamii ambazo Rais amesema asinge penda hilo litokee kwa sababu ni mwaka wa sensa angependa kujua idadi ya watu na makazi yao ili mipango ya maendeleo iweze kufanyika vizuri,”.

Aidha amefafanua kuwa kwa upande wa majengo ni sensa ya mara ya kwanza ambapo
serikali imelenga pia kutaka kujua hali halisi katika mazingira wanayoishi wananchi,uchumi wa kawaida wa mtanzania lakini kuweza kujua sasa itakuwa inawahudumia watu wenye hali zipi.

“Kwa sababu tupo tofauti wapo wenye maisha ya juu,ya kati na wale ambao yapo ya chini sana,kwaio kupata picha halisi ya mazingira ya watu wanayoishi unaweza kujua taifa unaloliongoza ni la namna gani, hii nayo inakwenda kusaidia hasa katika kukuza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja,”ameeleza Dkt Angeline.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Kivulini Yassin Aly ameeleza kuwa sensa ndio msingi wa takwimu mahususi za kuandaa mipango,mikakati ya kuandaa afua mbalimbali za kutokomeza mimba za utotoni,ndoa za utotoni na malezi hivyo jamii ishiriki kikamilifu.

“Zoezi hili uwa ni muhimu sana kwetu kwa sababu takwimu za sensa pia uwa zinaonesha idadi ya watoto ni wangapi wa kike na kiume na wanawake wangapi mipango yoyote ni lazima uainishe kwa makundi ili uweze kupanga vizuri mipango ya maendeleo,”ameeleza Yassin.

Naye Diwani wa Viti Maalum wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Sarah Lisso, amewahimiza wanawake wenzake kujiandaa kikamilifu katika kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi.

Pia wawe wahamasishaji kwa watu wengine ambao hawana elimu ya sensa,kwani zoezi hilo ni kwa ajili ya maendeleo ya watanzania wote.

“Endapo tutahesabiwa kikamilifu serikali yetu itakuwa na uwezo wa kufanya bajeti inayoenda miaka 10, bajeti hiyo itakuwa ni kamilifu kwa wale watu waliopo na watakaozaliwa kupitia sensa ya mwaka huu,”ameeleza Sarah.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula, akizungumza na wanawake wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikiwa ni kundi la tatu ambao wamepata mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022, na mapambano dhidi ya ukatili yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani hapa huku wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa shirika la Kivulini Yassin Ally.(Picha na Judith Ferdinand)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,akiwa katika picha baadhi ya wanawake wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikiwa ni kundi la tatu ambao wamepata mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022, na mapambano dhidi ya ukatili yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani hapa (Picha na Judith Ferdinand)