November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rubara: Mitaji midogo inachangia wachimbaji wadogo kutotumia wanajiolojia katika kazi zao.

Judith Ferdinand, Mwanza

Imeelezwa kuwa wachimbaji wadogo wa madini nchini wanataarifa juu ya uwepo wa taasisi ya kijiolojia Tanzania ila changamoto ni mitaji midogo walionayo ambayo inasababisha kushindwa kumudu gharama za kupata huduma.

Hayo yameelezwa na Meneja Mradi na Utafiti wa Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo(FADev),Evans Rubara,wakati akizungumza na Timesmajira online jijini Mwanza.

Rubara ameeleza,kuwa pamoja na kwamba mtaji wao hautoshelezi kulipa gharama za utafiti wa kijiolojia, wachimbaji wadogo kutokana na hali hiyo inapelekea kuwa wanajiolojia wenyewe katika maeneo ambayo wamepewa leseni ili kufanyia shughuli zao za uchimbaji.

“Wanahitaji sana sana kupata huduma kutoka kwa hao wataalamu wa sekta ya madini, hawawezi kumudu gharama za kuwalipa wataalamu kutoka kwenye taasisi ya kijiolojia Tanzania ili kuwafanyia hizi kazi,”ameeleza Rubara.

Rubara ameendelea kueleza kuwa unakuta mara nyingi wanaanza kuchimba duara hapa mara wanaenda futi kumi wengine wanaenda futi 20,wakikuta kwamba kama bado hawajafikia mwamba wanaacha.

Na wakati wanafanya hiyo shughuli ya kuchimba mashapu ya kuanzia unakuta wanapembua mchanga wanao upata wao wanasema wanapiga “chabo”.

Kwa maana kwamba wao wanachukua udongo walio upata wana uchekecha ili kuangalia kama kuna chembechembe za dhahabu na hawapati hivyo wangepata huduma kutoka kwenye taasisi ya kijiolojia Tanzania hakika wangepata faida zaidi na wangejua ni wapi pakuanzisha mashapu yao.

Hivyo ameeleza kuwa katika kutatua changamoto hiyo kwa wachimbaji wadogo
FADev,wameanza mjadala na taasisi ya kijiolojia Tanzania ili kuona ni kwa jinsi gani wanaweza wakawasaidia wachimbaji wadogo wenye leseni wanao fanya nao kazi.

Ili wawapatie huduma ya kufanya utafiti wa mali iliopo chini kwa bei nafuu au ambayo imepunguzwa kwa sababu hilo likifanyika wanaamini kwamba kwanza litachangia sana kwenye utunzaji wa mazingira.

“Mbali na uharibu wa mazingira wakati mwingine muda ni mtaji wanapoteza muda mwingi kuchimba sehemu moja na hawajapata chochote wanahamia sehemu nyingine kwa sababu amechimba sehemu moja lazima atumie rasilimali pesa kwa kile kidogo walicho nacho kwenye utafiti wao wa kawaida ambao wanafanya kwa nguvu zao,”ameeleza Rubara.

Meneja Mradi na Utafiti wa Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo(FADev),Evans Rubara.