November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othaman: Tuandike vitabu ili kujenga uelewa na kuacha historia kwa vizazi vyetu

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kuwa uandishi wa vitabu ni jambo jema katika kuakisi historia na maisha halisi ya jamii, ili kuendeleza urithi bora wa elimu na maisha mema kwa vizazi vijavyo.

Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani Jijini Zanzibar, mara baada ya kupokea Kitabu cha MAISHA YANGU, kilichoandikwa na Mwandishi Mzee Khamis Abdulla Ameir.

Amesema muendelezo wa urithi huo ni pamoja na azma ya viongozi na watu mashuhuri kuandika historia zao pamoja na za Nchi au jamii wanazotokea.

“Hii ni hazina kubwa ya nchi kwani inaweka wazi yale ambayo jamii inapaswa kuyatambua”, ameeleza Mheshimiwa Othman.

Mzee Khamis ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi mstaafu ameandika kitabu hicho kilichoakisi maisha yake halisi, historia ya kisiasa, Uchumi na Jamii kwa ujumla.

Kitabu hicho kimekabidhiwa kwa niaba, na binti yake Salma Khamis Abdulla ambaye ameambatana na Mohammad Yussuf Mshamba.

Naye, Mohammad Mshamba amesema kuwepo kwa historia za viongozi mashuhuri ni jambo la kujivunia katika muktadha wa historia ya Nchi.