November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania watakiwa kuungana na wito wa Rais wa kuhesabiwa katika Sensa ya watu na makazi

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Watanzania wametakiwa kuungana na wito wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wa kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi ya mwaka huu 2022.

Hayo ameyasema leo Spika wa Bunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania dkt Tulia Ackson wakati wa kongamano la kitaifa la viongozi wa Dini kuhusu sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 lililofanyika katika ukumbi wa mikutano Mwalimnyerere jijini Dar es salaam.

Dkt. Tulia amesema Sensa ya mwaka huu ni ya tofauti kwasababu inaangalia zaidi ya idadi ya watu na huduma zinazotolewa kwenye hayo maeneo ambayo watu wamehesabiwa.

Mbali na hayo Dkt. Tulia amesema Sensa ya mwaka huu itasaidia sana serikali kupata taarifa mbalimbali kwa maana ya umri wa watu ili wajue idadi kamili;

“Idadi ya watu tutakayoipata itasaidia mamlaka zetu za wilaya kutekeleza mipango yake kulingana na idadi ya watu waliopo huko kwasababu itaakisi pia matakwa yao”

Aidha Dkt. Tulia amesema Serikali inazo takwimu za jumla lakini bado ni muhimu kuhesabu kwasababu yapo mazingira ambayo serikali hayajapata taarifa

Dkt. Tulia amesema wanaamini Bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2023/24 itakua ya utofauti kwasababu watakua wamefahamu watanzania tupo wangapi na wabunge wanaowawaikilisha kutoka kwenye maeneo yetu wapo wangapi.

Spika wa bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson ametoa rai kwa viongozi wa dini kuendelea kuelimisha na kuhamasisha waumini wa dini zao kushiriki zoezi la sensa ili serikali iweze kuandaa dira ya maendeleo ya taifa pamoja na kuwa na mwelekeo mzuri wa kutoa huduma kwa jamii.

Amesema utoaji elimu na hamasa kwa jamii kuhusu ushiriki wa sensa ni muhimu kuzingatia makundi mbalimbali ikiwemo watu wenye ulemavu kuhakikisha jamii haiwafichi watu hao kwani haki ya makundi yote kushiriki zoezi la sensa.

Pia Dkt. Tulia amewataka wananchi wote kuendelea kufanya maandalizi ya kuhesabiwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya sensa kwenye jamii.

Kwa upande kamisaa wa sensa ya watu na makazi Anna Makinda alisema amesema suala la elimu kwa umma juu ya sensa ni endelevu hadi mwisho wa sensa hivyo ni wajibu na ni suala la uzalendo kwa kila mwananchi na viongozi wa dini kuhamasisha wananchi ushiriki wa zoezi hilo muhimu la kitaifa

Ameongeza kuwa sensa ya watu na makazi imewajali wananchi wa hali zote hivyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa watu wote wanaokwenda kuchukua taarifa zao ili kuweza kupata idadi iliyo kamili.

Mtoa mada kutoka ofisi Mtakwimu Mkuu wa serikali, amesema Sensa hii itakua ya kidigitali kwasababu shughuli zote zitakazofanyika zitakua zinatawaliwa sana na sayansi kwa maana ya kwamba makarani watatumia mifumo ya kielektroniki, nyenzo zitakazotumika katika sensa hiyo ni ramani ambapo ramani hiyo ni kwaajili ya kumsaidia karani wa sensa kuhakikisha kwamba hakuna mtu atakayehesabiwa zaidi ya mara moja lakini pia hakuna uwezekano wa karani kutoka nje ya eneo lake ambalo amepangiwa

Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum amesema sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa mustakabali wa ustawi wa nchi na maendeleo ya nchi pamoja na amani na usalama wa taifa la Tanzania na kuongeza kuwa waislamu wote wamelibeba jambo la sensa kwa ukubwa na kutoa ushirikiano wa kutosha lakini pia aliwaomba watanzania wote kwa pamoja kuwa tayari kuhesabiwa.

Askofu kutoka kanisa la Anglikana jijini Dar es salaam amesema sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 2012 kutokana na hilo ndani ya Taifa letu kuna mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hivyo kuwa na sensa kitaifa ni kutafuta kujitambua zaidi kwasababu sensa huleta umoja wa kitaifa zaidi na siyo utengano lakini pia hisia ya nguvu ya kizalendo kitaifa pasipo kujali itikadi na imani zetu.