November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto Korogwe wapaza sauti ukatili juu yao

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

NDOA za utotoni ama ndoa za kulazimishwa, watoto wa kike kupewa mimba katika umri mdogo, ukeketaji, vipigo, unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo watoto kubakwa au kulawitiwa, ubaguzi kwa misingi ya jinsia, rangi, dini ama misingi mingine na ajira za utotoni, ni ukatili dhidi ya watoto.

Ukatili dhidi ya watoto ni dhana pana ambayo inajumuisha kila aina ya unyanyasi anaoweza kufanyiwa mtoto. Zipo mila na vitendo vya kikatili katika jamii yetu ambayo hatuna budi kusimama kwa pamoja na kuvipinga kwa nguvu zote.

Hayo yalisemwa Juni 16, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Vision Tanzania Gilbert Kamanga kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika Kijiji cha Lusanga, Kata ya Mnyuzi, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, ambapo maadhimisho hayo yalifanyika kwa ngazi ya kiwilaya.

Akisoma hotuba ya shirika hilo kwa niaba ya Kamanga, Mratibu wa Mnyuzi AP, Samwel Charles, alisema maadhimisho hayo ya Siku ya Mtoto wa Afrika, yanatoa fursa ya kukumbushana kwamba ni wajibu wa Serikali, wazazi, walezi na kila mdau kuhakikisha kwamba kila mtoto katika jamii yetu analindwa dhidi ya mila ama vitendo hivyo viovu vinavyohatarisha usalama wake na hivyo kumzuia kufikia malengo yake kimaisha.

“Ukatili dhidi ya watoto ni dhana pana. Vitendo hivi ni pamoja na ndoa za utotoni ama ndoa za kulazimishwa, watoto wa kike kupewa mimba katika umri mdogo, ukeketaji, vipigo, unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo watoto kubakwa au kulawitiwa, ubaguzi kwa misingi ya jinsia, rangi, dini ama misingi mingine na ajira za utotoni, ni ukatili dhidi ya watoto” alisema Kamanga.

Kamanga alisema shirika hilo lisilo la kiserikali, limeweka mkazo katika kuwahudumia watoto, hasa wanaoishi kwenye mazingira magumu. Pamoja na mambo mengine, shirika lina kampeni maalumu ya kitaifa ya kupinga mimba na ndoa za utotoni.

Pia wanaamini, kila mtoto katika jamii ana haki ya kulindwa na kutengenezewa mazingira wezeshi ili waweze kuishi kwa usalama na kutimiza ndoto zake. Pia wanaamini juhudi za pamoja zinahitajika ili kutokomeza kabisa vitendo vyote kwa ukatili dhidi ya watoto.

Kamanga alisema, shirika hilo linatoa mchango muhimu katika kuimarisha ulinzi, usalama na ustawi wa watoto katika Wilaya ya Korogwe, na baadhi ya mambo yanayofanywa na shirika hilo ni kuwa wameanzisha na wanaendelea kuwezesha utekelezaji wa uandishi wa insha kwa wanafunzi wa darasa la sita na la saba.

Mashindano hayo yana lengo la kujenga uelewa kwa vijanarika na kuhamasisha mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni katika jamii. Mashindano hayo yanafanyika zaidi ya mikoa 10, ambapo program za maendeleo zinatekelezwa na shirika hilo.

“Hapa kwetu Korogwe, shindano limeshafanyika kwa ngazi ya shule, ambapo jumla ya wanafunzi 277 kutoka kata za Mnyuzi na Kwagunda wameshiriki kuandika insha. Washindi kumi kutoka kila shule, ambapo shule zilizoshiriki ni tisa, wameshapatikana.Washindi wa kwanza katika kila shule wamepewa fursa ya kuwasilisha insha zao mbele ya wanafunzi wengine, ambapo jumla ya wanafunzi 3,144 walipata fursa ya kusikiliza jumbe hizo.

“Tunashirikiana na Serikali katika kuimarisha Kamati za MTAKUWWA (Mpango wa Taifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto) katika za vijiji na kata. Kamati za vijiji vyote 12 vilivyo katika eneo la mradi zimeundwa na kujengewa uwezo. Kamati hizi zina jukumu la kuhakikisha usalama wa watoto katika jamii, sambamba na kuripoti kwenye mamlaka husika, vitendo vyote vya ukatili dhidi ya mtoto pale vitakapojitokeza” alisema Kamanga.

MTAKUWWA unatekelezwa nchini Tanzania kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/18 hadi 2021/22, ambao upo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

Akisoma risala ya watoto, mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Mnyuzi Joyce Msuya, alisema kauli mbiu ya mwaka huu “Tuimarishe ulinzi wa mtoto; tokomeza ukatili dhidi yake, jiandae kuhesabiwa”, ina maana kubwa kwao.

“Kauli mbiu hii ni muhimu sana kwetu sisi watoto. Lengo la kauli mbiu hii ni kuwahimiza wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kulinda haki zetu sisi watoto na kutokomeza ukatili dhidi yetu. Pia jamii kwa ujumla tunawakumbusha kupitia kauli mbiu hii kujitokeza kuhesabiwa wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022” alisema Msuya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Kijiji cha Mzindawa, ambaye pia ni Mjumbe wa MTAKUWWA kwenye kata za Kwagunda na Mnyuzi, Hamdan Faraji, alisema moja ya mambo yanayochangia watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili kwenye jamii, ni jamii hiyo kutetea uovu. Mtoto anaweza kupewa mimba, lakini aliyefanya kitendo hicho akatetewa.

“Mtoto anafundishwa kusema uongo kwa mtu aliyempa mimba. Kuwa ni mtu mmoja alikuja na Fuso la kijani kuchuma maembe au machungwa. Sasa tunajiuliza hilo Fuso la kijani na huyo mtu tutawapata wapi! ukichunguza, kumbe aliyempa mimba yupo hapo kijijini, na ndugu wa pande zote wameshakubaliana kumficha” alisema Faraji.

Akisoma hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Halfan Magani, ambaye ndiyo alikuwa mgeni rasmi, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo David Mpumilwa, alisema baadhi ya wazazi wanachangia kuharibu tabia za watoto ikiwemo kugombana ama kutoa matusi mbele yao.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Fumbo iliyopo Kijiji cha Gereza, Kata ya Kwagunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wakionesha mabango yanayopinga ukatili dhidi ya watoto. Ni kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika ngazi ya wilaya kwenye Kijiji cha Lusanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Wanafunzi wa shule za msingi kwenye kata za Mnyuzi na Kwagunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wakifanya maandamano, wakionesha bango linalopinga ukatili dhidi ya watoto. Ni kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika ngazi ya wilaya kwenye Kijiji cha Lusanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Mratibu wa Mnyuzi AP Samwel Charles akisoma taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Vision Tanzania Gilbert Kamanga kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika ngazi ya wilaya kwenye Kijiji cha Lusanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Mratibu wa Mnyuzi AP, Shirika la World Vision Tanzania, Samwel Charles (kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto wa shule za msingi kata za Mnyuzi na Kwagunda ambao walifanya vizuri kwenye masomo yao, na shirika hilo kuwapa zawadi ya mabegi ya shule. Ni kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika ngazi ya wilaya kwenye Kijiji cha Lusanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).

Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwenye kata za Mnyuzi na Kwagunda, wakiwa kwenye picha ya pamoja katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika ngazi ya wilaya kwenye Kijiji cha Lusanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwenye kata za Mnyuzi na Kwagunda, wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa wilaya na Shirika la World Vision Tanzania katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika ngazi ya wilaya kwenye Kijiji cha Lusanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).