Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa hali ya unyanyapaa kwa watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi kwenye jamii hususani nyumbani bado ni changamoto.
Hayo yameelezwa na Wakili Tiba wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi(NACOPHA) Konga ya Nyamagana Ellyangel Lawrence wakati wa siku ya maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika,ambayo uadhimisha kila ifikapo Juni 16 ambapo kimkoa imefanyika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Ellyangel ameeleza kuwa jamii na familia imekuwa inawatenga sana watoto hao wakisha fahamu kuwa wanaishi na maambukizi ya VVU kwa kuwatengea vyombo vyao pekee huku wakikosa haki ya kusoma.
“Unyanyapaa unaotokea kwenye jamii hususani katika nyumba zetu ni kwa wazazi wengi wanawaficha watoto wao wanaoishi na maambukizi kwa kushindwa kuwaeleza ukweli kuwa wanatumia dawa za VVU na badala yake wanawaambia ni dawa za akili hali inayomjengea mtoto akikua anaacha kutumia dawa hivyo kuugua na mwisho wa siku anakuja kugundua anaamua kuchukua maamuzi ya kwenda mbali na familia au kujiua,”ameeleza Ellyangel.
Kwa upande Wakili Tiba kutoka NACOPHA Konga ya Nyamagana Lilian John, ameeleza kuwa unyanyapaa mwingi unaotokea kwa watoto hao unasababisha vitendo vya ukatili kwa watoto.
Lilian ameeleza kuwa amii inatakiwa kupata elimu ili kuondoa vitendo vya ukatili kwa watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi na pia kuweza kuona watoto hao kama wa kawaida.
Pia ameeleza kuwa wazazi na jamii wanapaswa kuwaweke wazi watoto wao tangu siku walipogundua kuwa mtoto anaishi na maambukizi ya VVU huku wakisha tambua hali ya mtoto wampeleke katika vituo vya afya ili aweze kupata huduma za afya na aweze kukutana na wenzie na asijuone mpweke.
“Watoto wanapofichwa wanajiona wapo pekee yao hawana ujasiri wa kusema wala kutambua haki zao kwani wanakuwa wamefungiwa katika nyumba hivyo jamii iweze kuwatoa nje na iwapeleke katika vituo vya afya waweze kupata tiba,” ameeleza Lilian.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli,aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel katika maadhimisho hayo,amesema ni muhimu jamii kushiriki vizuri ili kutokomeza ukatili wa watoto.
“Wazazi na walezi wote tushirikiane kuhakikisha tunakomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni dhairi kuwa watoto kwa hivi sasa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kutokana na matatizo ya kifamilia yanayosababisha malezi duni,” ameeleza Kalli.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM