November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Kibondo aanika faida za mafunzo kwa wakulima yaliyotolewa na WFP

Na David John, TimesMajira Online

MKUU wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Kanali Aggrey Magazwa amesema shirika la Mpango wa Chakula Duniani(DWF) linamchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya kilimo na wakulima ndani ya Wilaya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ziara ya kutembelea mradi wa UN Kigoma Pamoja unaohusisha mashirika 16, Kanali Magazwa amesema kupitia mradi huo WFP wamejikita katika eneo la kilimo.

“WFP inamchango mkubwa sana kwenye wilaya yetu ya Kibondo katika eneo hili la kilimo.Kwanza inatoa mafunzo kwa wakulima jinsi ya kupanda,kuvuna na kuhifadhi mazao.Wamenunua mashine za kupuchukua mahindi na wamekarabati maghala.Pia wamekuwa wakijihuhisha na ununuzi wa mazao ya wakulima wetu.

“Mkulima yoyote kitu ambacho anakipenda ni kuwa na uhakika wa soko wa kile ambacho anakizalisha. Tunawashukuru WFP kwani mbali ya kutoa mafunzo ya kulima kilimo chenye tija wamewafanya wakulima kuwa na soko la uhakika na bei yao iko juu ukulinganisha na wanunuzi wengine,”amesema Kanali Magazwa.

Akielezea zaidi kuhusu WFP, amesema anawashukuru kwa kutoa mafunzo kwa wakulima na hata ukipita mashambani unaona namna ambavyo wakulima wanalima kisasa,

“Kutokana na mafunzo ambayo wakulima wetu wameyapata katika wilaya yetu ya wakulima wamepata chakula licha ya kutokuwa na mvua za kutosha kwa msimu huu. Hivyo tunaomba WFP waendelee kuwasaidia wakulima.Pia tunaomba waendelee kununua mazao ya wakulima,”amesisitiza.

Alipoulizwa wamejipangaje kuhakikisha wanaendelea na program hiyo iliyoanzishwa na WFP, Kanali Magazwa amsema wamejipanga vizuri kwani mafunzo yanayohusu kilimo yalianza kutolewa kwa maofisa ugani wao.

“Hivyo kwa kutumia watalaamu wetu watakuwa wakipata sehemu ambazo hawajafikiwa na WFP lakini wakulima waliopata mafunzo nao wataelimisha wengine, lakini halmashauri imejipanga, na mpango upo.

Awali akizungumza na waaandishi wa habari waliotembelea mradi wa UN Kigoma Pamoja katika eneo la kilimo, Mkuu wa WFP Wilaya ya Kibondo Said Johari amesema kupitia mradi huo wameshiriki kikamilifu kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo chao.

Amesema kiasi cha Sh.bilioni 5.1 zimetumika kufanikisha mradi na baadhi ya sehemu ya fedha zimetumika kutoa mafunzo kwa wakulima, maofisa ugani wa halmashauri zote zenye mradi, kujenga maghala na kununua mashine za kupukuchukua mahindi.

“Kwa wilaya ya Kibondo wakulima wengi wamenufaika na mradi huu wa UN Kigoma Pamoja katika eneo hili la kilimo.Mradi wetu unaisha Juni 30 mwaka huu lakini kuna uwezekano wa kuendelea na hatua ya pili, lengo ni kumsaidia mkulima.”

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Kanali Aggrey Magwaza akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo) pichani kuhusu manufaa yaliyopatikana kutokana na uwepo wa mradi wa kuendelea wakulima kupitia Mradi wa UN Kigoma Pamoja ambapo WFP katika mradi huo wameamua kusimamia kilimo kwa kuendeleza wakulima.
Mkuu wa WFP Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma Said Johari akielezea jambo kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mradi wa kuendeleza wakulima katika Wilaya hiyo unaofadhiliwa na WFP.