Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Tanzania na Italia zimeahidi kushirikiana kukuza na kuendeleza sekta ya biashara ya uwekezaji kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Italia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alisema Tanzania imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kuwasihi wafanyabiashara wa Italia kuja kuwekeza nchini kwa kuwa ni salama zaidi.
Balozi Mulamula aliongeza kuwa, Tanzania na Italia zimekuwa na utamaduni wa kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kupitia majukwaa mbalimbali ya biashara na matokeo chanya ya majukwaa hayo yameanza kuonekana ambapo Disemba, 2021 kupitia kongamano la biashara na uwekezaji lililofanyika Italia, kampuni ya Kiitaliano ‘Suness Limited’ inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ilisaini makubaliano na Shirika la Taifa la madini (Stamico) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa shaba inayopatikana Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi ameipongeza Tanzania kwa jitihada kubwa za kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini.
Aliongeza kuwa kitendo cha Tanzania kuviondoa vikwazo vya biashara kimeongeza imani kubwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wengi duniani kuiona Tanzania ni salama. Aidha, Balozi Lombard alimpongeza Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuimarisha Diplomasia ya Uchumi na mataifa mengine duniani.
Tanzania na Italia zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja za kilimo, afya, elimu, maji, nishati, utalii na maendeleo ya sekta binafsi.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia