December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi 5,621 Bumbuli kupata huduma ya majisafi

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Bumbuli

MRADI wa Maji Mayo katika Halmashauri ya Bumbuli, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga unaotarajiwa kukamilika Juni, 30, mwaka huu, utanufaisha wananchi 5,621 wa vijiji viwili vya Mayo na Kizanda.

Hayo yameelezwa kwenye taarifa ya ujenzi wa miundombinu ya mradi huo na Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma.

Ni baada ya kiongozi huyo kufika Juni 3, 2022 katika Kijiji cha Kizanda na kukagua mradi huo kabla ya kuweka jiwe la msingi, ambapo hadi kukamilika kwa mradi huo utagharimu sh. milioni 531,893,820, ambapo sh. milioni 430,909,580 ni gharama za mkandarasi na sh. milioni 100,984,240 ni gharama za ununuzi wa mabomba ya mradi huo.

“Mradi wa Maji Mayo ulianza kutekelezwa Februari mosi, 2022, na unapaswa kukamilika Juni 30, 2022 kwa lengo la kuwapatia maji wakazi 5,621. Ujenzi wa mradi unahusisha jumla ya vijiji viwili vya Mayo na Kizanda katika Kata ya Mayo, na kazi zilizopangwa kutekelezwa kwenye mradi huu ni ujenzi wa chanzo kipya cha maji.

“Ufyekaji wa njia za bomba kuu, uchimbaji wa mitaro ya bomba yenye urefu wa mita 15,000, ulazaji na uungaji wa mabomba mita 9,140, ujenzi wa chemba pamoja na vifaa vyake, ujenzi wa BPT (matanki madogo yakupunguza kasi ya maji) mawili, ujenzi wa tanki la maji lita 90,000, na ujenzi wa vituo vinane (8) vya kuchotea maji (vilula), na utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 50, na unategemewa kukamilika Juni 30, 2022” alisema Sizinga kwenye taarifa hiyo.

Sizinga alisema changamoto iliyopo katika utekelezaji wa mradi huo ni mazingira magumu ya kupandisha vifaa na malighafi za ujenzi, na hali ya mvua katika eneo la ujenzi kwa mwezi Aprili.

Mradi wa Maji Mayo ambao unatekelezwa na RUWASA Wilaya ya Lushoto, ni mmoja wa miradi nchini ambayo inajengwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19.

Sehemu ya mabomba ya Mradi wa Maji Mayo yatakayopeleka maji kwenye vijiji vya Mayo na Kizanda. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro (wa pili kushoto) akizungumza na wananchi mara baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma (wa pili kulia) kuweka jiwe la msingi Mradi wa Maji Mayo. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lushoto Rashid Shekalata. (Picha na Yusuph Mussa).