Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tanga
Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA) imekiri kuwepo kwa mafanikio makubwa tangu alipoingia madarakani Rais Samia hususani ongezeko la muitikio wa watu wa kusajili makampuni, majina ya biashara sambamba na kupata leseni za biashara zao.
Akizungumza na Times Majira Msajili msaidizi kutoka Brela Seleman Seleman, kwenye maonyesho ya 9 ya biashara na utalii yanayofanyika jijini Tanga ambapo wamekuwa wakitoa elimu juu ya umuhimu wa wananchi kusajili biashara zao.
Seleman amesema kuwa kwa kipindi kimoja tokea Rais Samia alipoingia madarakani wameweza kusajili makampuni 11422 ambapo kwa najina ya biashara wameweza kusajili majina ya biashara 22251 lakini pia alama za biashara wamesajili 3056 ambapo katika leseni za kundi A wametoa leseni 12704.
“Kwa kipindi hiki kimoja cha mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kimeonyesha mafanikio makubwa ukilinganisha na vipindi vingine jambo ambalo limeonyesha ari kwa watu kusajili makampuni, majina ya biashara lakini pia kupata leseni za biashara zao, “alisisitiza Seleman.
Aidha amesema kuwa hali hiyo pia imewaongezea ari wao kama watendaji wa Brela ambapo kupitia matamasha mbalimbali wanashiriki ili kuifikia jamii ambapo walengwa wakiwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
“Wito wangu kwa wafanyabishara kabla ya kuanza kufanta jambo wawe wanapitia na kutafuta taarifa kwanza kwa wahusika ambao ni Brela kupitia mitandao ya kijamii au website zetu zinazoeleza sisi tunafanya nini na ikiwa kama kuna sehemu mtu hajaelewa kuna namba ya huduma kwa wateja hivyo watu wanaweza kupiga na kupata taarifa sahihi hii itawapunguzia wateja kupewa taarifa na watu ambao si sahihi, “alibainisha Seleman.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Tanga waliotembelea banda hilo la Brela aliwemo Richard Otto amesema jambo la kwanza lililompeleka ni kutaka kujua namna ya kusajili jina la biashara na kampuni kwa kuwa alikuwa hajui umuhimu wa kusajili biashara yake.
“Nilichonufaika nacho baada ya kufika hapa Brela ni kurasimisha biashara hasa kwa sisi vijana ambao tumekuwa rukifanya biashara bila kusajili na hivyo kushindwa kutambulika nashukuru nimepata suluhisho na njia za kufanya mwanzoni huu mfumo ulikuwa unasumbua pale ulipoanzishwa mfumo wa usajili online lakini sasa ivi nimeambiwa taratibu zimekaa vizuri, “alisema, Otto.
Veronica Temu naye ni mmoja wa wakazi wa wilaya ya Korogwe alisema amefurahia kwa kuwa anaweza kufanya, usajili huo kwa kutumia simu yake au kompyuta akiwa nyumbani kwake na hivyo imewarahisishia kwa kiwango kikubwa.
More Stories
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta