December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAC yawakumbusha wamiliki wa vyombo vya usafiri majini

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

LICHA ya elimu inayoendelea kutolewa na Shirika la uwakala wa Meli Tanzania’TASAC’ kwa wasafiri na wamiliki wa vyombo vya usafiri majini bado muitikio na utekelezaji wa maagizo mbalimbali yanatolewa umekuwa mdogo kwa wananchi hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya watu .

Hayo yameelezwa na afisa mfawidhi kutoka shirika la uwakala wa Meli Tanzania mkoa wa Tanga ‘TASAC’ kapten Christopher Shalua wakati akiwa katika maonyesho ya 9 ya utalii na biashara yanayofanyika mkoani hapa ambapo alisema shirika hilo linaelekeza na kutoa katozo kwa wamiliki wa vyombo vya vya kusafirisha abiria kutokutumia kusafirisha binadamu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ili kuweza kuepukana na athari ambazo zinaweza kujitokeza na hatimaye kughalimu maisha ya binadamu.

“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wasafiri na wamiliki kuhakikisha kuwa hawahatarishi maisha ya watu ikiwemo matumizi sahihi ya vifaa lakini bado muitikio sio mzuri sana kwa wananchi na wamiliki wa vyombo lakini Hata hivyo tumekuwa tukijitahidi mara kwa mara tunarudia kutoa elimu ili iweze kuwasaidia”alisema Shalua

Alisema wamekuwa wakiitumia kamati za ulinzi na usalama kudhibiti bandari bubu ambazo zimekuwa zikitumika kusafirisha abiria pamoja na mizigo kwa njia zisizo rasmi na kuwashirikisha viongozi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha wanashirikiana katika kudhibiti abiria kutumia vifaa ambavyo havijaruhusiwa.

“Kisheria mtendaji wa kijiji au mtaa ana wajibu wa kuhakikisha kwenye eneo lake kuna usalama na vyombo vile ambavyo haviruhusiwi kubeba abiria havipokei katika mtaa wake lakini pia na wakuu wa wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama nao tumekuwa tukiwatumia barua kwahiyo tunawategemea sana katika kutekeleza agizo hilo” aliongeza.

Kwa upande wake afisa Uhusiano mwandamizi kutoka shirika hilo Amina Miluko alisema kuwa kwa kuzingatia majukumu yao wamekuwa wakifwatilia bandari zote hapa nchini ikiwemo bandari kavu kwa lengo la kuhakikisha usalama wa raia na kudhibiti mianya yote ya usafirishaji unaokiuka sheria.

Aidha aliwataka wananchi pamoja na wamiliki wa vyombo vote vya usafirishaji wa mizigo pamoja na abiria kufuata sheria za usafirishaji hapa nchini sambamba na kurasmisha bandari zote bubu.

“Kikubwa tunachokifanya ni kuendelea kushirikiana na mamalaka ya bandari hapa nchini kutoa elimu kwa wananchi pamoja na wamiliki wa vyombo ambapo ni pamoja na kukagua vyombo vyote vinavyotumika kwa kupanga au kustukiza na kuhakikisha kuwa bandari zote bubu zilizopo zinafuata sheria kwa kurasimishwa” alisema Mwiluko.

Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Amina Miluko atoa maelezo kwa mkuu wa mkoa wa Tanga,Adam Malima alipotembelea banda lao