Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Ruangwa
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa {NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Rais Samia Suluhu Hassan sasa anakirejesha Chama kwenye zama za ujamaa na kujitegemea kama ilivyoasisiwa na viongozi wa taifa wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Amesema hayo jana aliposhiriki ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Namichiga, katika Halmashauri ya Wilaya ya, Ruangwa akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Lindi kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na uhai wa Chama ambapo alieleza kufurahishwa kwake na ushiriki wa wananchi katika ujenzi huo kwa kujitolea.
“Mwenye kokoto, mwenye simenti, mwenye kila kitu tunakwenda kuunga nguvu ujenzi wa taifa ili kufikia maendeleo kwani hatuna mjomba, hatuna shangazi, hatuna mama mdogo atakayetoka anakotoka aje atufanyie kazi ya kujenga maendeleo kwa umoja wetu, mchango wetu ni muhimu ili Chama hiki kuhakikisha kimesimama.
“Wazee wetu walifanya haya tunayoyafanya sisi (kujitolea nguvu). Nimefarijika sana na kinamama mnavyotisha katika kushika hatamu za kuongoza nchi kama ambavyo Rais Samia anafanya, lakini mnatisha kwenye kuhamasisha maendeleo.
“Wakinamama kwenye ujenzi wamekuwa wengi zaidi, kwenye uhamasishaji wamekuwa wengi zaidi, kwenye kutuongoza wanafanya vizuri zaidi kama anavyofanya Rais Samia, Mungu awabariki sana, Mungu awalinde sana mama zetu kwa namna ambavyo mnaleta ari na shime ya maendeleo kwenye taifa hili,” anasema.
Kuhusu kasi ya maendeleo Shaka amesema yako pale pale na kwamba kutokana na kutambua mchango wa wakulima serikali ya awamu ya sita itaendelea kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo ili ilete tija kwa kila mkulima nchini.
Amesema anatambua kuwa huko nyuma kulikuwa na changamoto katika kilimo cha zao la korosho, lakini serikali chini ya Rais Samia imeendelea kuzitafutia ufumbuzi. Kwa mujibu wa Shaka, miongoni mwa utatuzi wa changamoto hizo ni pamoja na kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima wa korosho ambazo zitagawiwa bure kwa wakulima wa zao hilo.
“Nipongeze mpango wa serikali wa kutoa pembejeo bure kwa wakulima, Rais Samia anafanya maendeleo bila kubagua na bahati nzuri Mbunge wenu ( Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa) naye anafanya kazi nzuri ya kuhakikisha anawatetea wananchi wa Ruangwa.
Serikali ya CCM awamu ya sita chini ya Rais Samia itaendelea kutatua changamoto na kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuongeza fedha za maendeleo katika kila sekta mfano mzuri nimeelezwa hapa Wilaya ya Ruangwa huko nyuma ilikua inapata shilingi milioni 400 kwa ajili ya miradi ya barabara, lakini sasa imepokea zaidi ya shilingi bilioni 1.5, hakika chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kazi inaendelea tena kwa kasi kubwa.” alisema.
More Stories
Rehema Simfukwe atoboa siri sababu kuimba wimbo wa Chanzo
Tanzania ipo tayari kupokea wakuu wa nchi,mkutano wa nishati-Dkt.Kazungu
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano