Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Serikali kupitia wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari imelitaka shirika la posta nchini kuzingatia utoaji wa huduma zenye ubora kwa kuzingatia mifumo ya kidigitali ikiwa ni pamoja na biashara mtandao ili kuleta tija kwa Taifa na kuongeza mapato.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 30, 2022 na Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo, Nape Nnauye wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya kibiashara kati ya Shirika la Posta nchini Tanzania na Shirika LA Posta Oman.
Alisema kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza masoko baina ya mataifa hayo mawili. Nape alisema uwepo wa ushirikiano huo utasaidia nchi zote mbili kuboresha huduma zitakazowalenga wananchi moja kwa moja kutokana na kodi zinazopatikana zitatekeleza miradi ya kimkakati.
“Ushirikiano huu ni wa manufaa kwa pande zote mbili na manufaa hayo hayaishii kwenye taasisi tu, bali unaenda hadi kwenye Serikali zetu, hivyo ni matumaini yangu kwamba tutaimarisha ushirikiano huu na kuona kwamba kwa pamoja tunafaidika,” alisema Waziri Nape na kuongeza;
“Ushirikiano huu utaimarisha utoaji huduma inayoendana na Teknoloji ya kisasa hivyo kuimarisha shughuli za Posta na kuzitambulisha, kuzitangaza huduma mbalimbali za Posta Duniani kote,” alisema.
Waziri Nape alisema huduma za Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta la Oman yakiwemo maduka mtandao, yanaenda kuimarika zaidi kwakuwa wananchi wataagiza na kuuza bidhaa zao kwa urahisi sana hasa kwenye biashara zinazofanyika kati ya nchi hizi mbili
Waziri Nape alizipongeza pande zote mbili kwa utayari wa kushirikiana kwenye utoaji wa huduma kwa wananchi ,lakini pia kwa kupanua wigo wa huduma wanazozitoa ndani ya nchi na nje ya mipaka ya nchi zetu.
Kwa upande wake, Posta Masta Mkuu kutoka Shirika la Posta Nchini Tanzania, Macrice Mbodo alisema makubaliano hayo yatajikita katika maeneo 17 ambayo si tu yanalenga kuleta utendaji kazi lakini pia kupanua wigo na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa mashirika hayo duniani kote.
“Tunakwenda kushirikiana katika uunganishwaji wa maduka mtandao ambapo pamoja na kuwa litaongeza mapato kwa shirika, ushirikiano huu utawezesha Watanzania kununua na kusafirishiwa bidhaa ndani na nje ya nchi zinazouzwa na kununuliwa kupitia majukwaa ya kibiashara mtandao kote duniani yatakayokuwa yameunganishwa na majukwaa mengine mtandao ya Posta ya Oman, tanzania na majukwaa mengine ya kimataifa,”alisema.
Aidha alisema watashirikiana katika Kubadilishana ujuzi na teknolojia utoaji wa huduma za posta kwa wananchi ambapo katika eneo hilo posta ya Tanzania na posta ya Oman itabadilishana ujuzi na teknolojia ya utoaji huduma za posta kwa wananchi kama vile usafirishaji wa barua, nyaraka, mizigo na sampuli za maabala, huduma za utumaji fedha na uwakala, biashara ya mtandao na huduma nyinginezo.
Aidha watashirikiana kwa kuandaa na kuchapisha stemp za pamoja za vivutio vinavyopatikana Tanzania na Oman ambazo zitauzwa Duniani kote kupitia mitandao ya uuzaji wa stemp ambapo zitatumika kutangaza vivutio mbalimbali vinavyopatikana hapa tanzania na hivyo kuwavutia watalii kutoka nchi mbalimbali duniani kutembelea nchi yetu.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba