November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muheza ‘waupiga mwingi’ miradi ya Mwenge

Na Hadija Bagasha Tanga, Halima

Wilaya ya Muheza imefanikiwa kupitishiwa miradi yake yote nane iliyozinduliwa, kukaguliwa na kuwekewa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru Mwaka 2022.

Hiyo ni hatua kubwa kulinganisha Wilaya ya Tanga Mjini na Mkinga ambako Mwenge wa Uhuru ulipita na baadhi ya miradi ilikataliwa.

Miradi hiyo yenye thamani ya Sh bilioni 1.7 ni pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba nne za walimu katika Shule ya Sekondari Misozwe, kukabidhi samani kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Mbaramo ambazo fedha zake zinatokana na michango ya mwenge, uwekaji jiwe la msingi katika ukumbi wa matukio ya kijamii wa Muheza Comfort na nyumba tatu za watumishi katika Hospitali ya Wilaya ya Muheza.

Miradi mingine ni ule wa maji Mizembwe uliopo katika Kijiji cha Pangamlima, Mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mkumbi-Muheza Estate katika Kijiji cha Tanganyika yenye urefu wa Km moja moja iliyogharimu Sh milioni 498.54 ambao umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika Juni 10, mwaka huu na kukagua Klabu ya Vijana Wapinga Rushwa katika Shhule ya Sekondari Chief Mang’enya na Kikundi cha Vijana kinachojihusisha na kuchakata mkonge cha Mkonge Kwanza katika Kata ya Kwemkambala.

Haikuwa kazi rahisi kupitishwa kwa miradi hiyo kutokana na baadhi yake kuwa na dosari ndogo ndogo ikiwamo kutoshirikisha Mkurugenzi wa halmashauri ambaye ndiye muidhinisha fedha za miradi hiyo ambapo Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Sahili Geraruma aliwaonya wasimamizi wa miradi kujitathmini na kufuata utaratibu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akiwa katika mradi wa ujenzi wa nyumba nne za walimu katika Shule ya Sekondari Misozwe wilayani humo uliogharimu Sh milioni 116,345,000 alisema ameridhishwa na mradi huo huku akitoa maelekezo kwa baadhi ya maeneo kufanyiwa marekebisho.

“Nawasihi wanaopewa dhamana ya kusimamia miradi kujitathmini, kuacha dharau na kufuata utaratibu kama una nyaraka inatakiwa kusainiwa na Mkurugenzi basi apewe kuepusha sintofahamu katika miradi yenu.

“Lakini na ninyi viongozi nawasihi mlisimamie hili, marekebisho yafanyike, wasimamizi warekebishe mradi utekelezwe kwa viwango vinavyotakiwa,” amesema Geraruma.

Aidha, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Mizembwe Kijiji cha Pangamlima ambapo kabla ya kuzinduliwa, Geraruma alitaka kuona chanzo cha maji hayo ambacho kilikuwa umbali wa zaidi ya Km 15 ambapo alikwenda na wasimamizi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya na Mbunge wa Muheza, Hamisi Mwinjuma.

“Kwanza tunaomba radhi kwa muda tulioutumia kuangalia chanzo cha maji lakini tumefanya vile kwa ajili ya kuangalia fedha za serikali kama zimetumika kwa malengo kusudiwa. Nawapongeza katika suala zima la kutunza mazingira, kuna vyanzo vya maji vya kutosha nitashangaa siku nikija Muheza nikakuta kuna changamoto ya maji.

“Nimekwenda Pangamlima kuangalia chanzo cha maji haya nimekuta maji yanamwagika yaani maji yapo ya kutosha pongezi kwa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia mradi huu.

Myatunze vizuri vyanzo vyetu, kwa jinsi maji nilivyoona mnaweza kuoga hata mara nne maji yanatosha,” alisema.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo alisema mradi huo ulibuniwa mwaka 2018 na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa maji katika vijiji vya Miyanga, Zeneti na Mbwembwela ambavyo kwa pamoja vinaunda jina Mizembwe ambao umegharimu Sh milioni 995.4 na mradi umefikia asilimia 92 ya ujenzi wake.

“Ujenzi wa chanzo cha maji umekamilika, vituo 10 vya kuchotea maji vimekamilika na huduma imeanza kupatikana tangu Mei mwaka huu na unahudumia watu 4,432,” alisema.

Akiwa katika mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mkumbi-Muheza Estate unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) ya Km moja iliyogharimu Sh milioni 498.54 ambao umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika Juni 10, mwaka huu alimtaka mkandarasi kuzingatia muda uliowekwa ili mradi ukamilike kwa wakati bila kuomba kuongezewa muda mwingine huku akimtaka mkaguzi wa ndani kujitathmini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo alisema amepokea maelekezo na kuahidi kuyasimamia na kuyafanyia kazi ikiwamo kuifanyia marekebisho miradi yenye dosari ndogo ndogo ili ikamilike kwa wakati.