November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya wananchi elfu nane wilayani ChakeChake hatarini kupata maradhi ya mlipuko

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Zaidi ya wananchi elfu nane wa vijiji tisa vya shehia ya Ndagoni Wilaya ya Chake Chake wako hatarini kupata maradhi ya mripuko kwa kutumia maji ambayo si safi wala salama.

Wakizungunza kijijini kwao baadhi yao akiwemo Amina Mohamed, Nassor Khamis na Fatma Suleiman wamesema ni miezi miwili hawapati maji kutoka mferejini, na wanatumia maji kutoka katika visima vya asili na kwenye mashimo mabondeni maji ambayo si salama.

Wamefahamisha kuwa hulazimika kutoka majumbani kwao usiku kwenda kuweka foleni ya maji na kuwaacha watoto wao ndani bila ya kuwa na mtu wa kuwaangalia.

Sheha wa shehia ya Ndagoni Massoud Ali Mohamed amekiri kuwepo kwa tatizo la maji katika vijiji hivyo na tayari wameshafuatilia katika mamlaka ya maji zawa.

Amesema baada ya kufuatilia katika mamlaka hiyo wameambiwa kuwa tatizo ni umeme ni mdogo ambao unasukuma kutoka kwenye kisima kupeleka majumbani.

Kufuatia malalamiko ya wananchi hao juu ya suala la maji , Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji ofisi ya Pemba Omar Mshindo Bakar amesema tatizo limeripotiwa kwa muda wa wiki mbili zilizopita nyuma na baada ya kwenda wamegunduwa tatizo sio kwa zawa bali linahusu miundombinu ya umeme.

Afisa Uhusiano wa umeme ZECO Pemba Amour Salum Massoud amesema mafundi wao wanaendelea kufuatilia kwa karibu tatizo hilo eneo hilo na kulifanyia matengenezo.