Na Mwandishi Wetu ,Timesmajira,Online,Namtumbo
MWILI wa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kujitegemea jijini Mbeya, Hannerole Mrosso (33) umezikwa jana katika makaburi ya Nandungutu, Kijiji Cha Mtonya,kata ya Likuyu, wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Marehemu Hannerole alifariki dunia Mei 13, mwaka huu katika hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya, kitengo cha huduma ya mama na mtoto Meta wakati akijifungua.
Akizungumza mara baada ya kusoma dua katika mazishi hayo sheikh wa kata ya Rwinga, Zuberi Lembuka, alisema kifo Cha Hannerole kiwe funzo kwa watu wengine kujitathmini maisha yao ya duniani ili kujitayarisha na kuwa tayari siku watakapofikwa na mauti.
Amesema Kila mmoja wetu ataulizwa na mwenyezi Mungu mema aliyoyafanya duniani na lazima awe na majibu, hivyo ni vyema watu waliopata bahati ya kuwa hai kutumia muda uliobaki kutenda mema na kumrejea muumba wao kabla ya kiama kufika.
“Kuna maswali utaulizwa siku hiyo, lakini kwa waislamu, tunawakumbusha kuwa ukiulizwa siku hiyo ya kiama kuwa mama yako ni nani? Jibu lake ni Quran, na hayo majibu hayaji hivi hivi tu, ni lazima uishi na utende maisha mema ambayo yanampendeza Mwenyezi Mungu, kwa mtindo huo utakuwa na majibu mazuri siku hiyo” alisema
Nae Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Mitiulaya, Mussa Mohamed aliwashukuru waandishi wa habari wa mkoa wa Mbeya kwa kujitoa kwao kuanzia kwenye shughuli ya kuuaga mwili wa mpendwa wao hadi kushiriki kwenye mazishi.
Mohamed ambaye Pia alikuwa mwakilishi wa familia kwenye shughuli hiyo amesema kujitoa kwa watu katika tukio la msiba wa mwanao inadhihirisha namna alivyokuwa akishirikiana vizuri na wenzake wakati wa uhai wake.
Katibu wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Mbeya (MBPC) Keneth Mwakandyali amewashukuru wadau wote waliojitoa kwa hali na mali hadi kuhakikisha Marehemu anapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.
More Stories
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha
Wahakikishiwa usalama siku ya kupiga kura
CCM inabebwa na kazi nzuri za Rais Dkt. Samia-Makalla