Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amewataka Maafisa na Askari wa Uhifadhi waliohitimu mafunzo ya kijeshi kuhakikisha wanalinda vivutio vya utalii vilivyopo nchini na kuongeza kuwa Filamu maarufu ya ‘The Royal Tour’ iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan haitakuwa na maana kama vivutio hivyo havitalindwa
Naibu Katibu Mkomi ameyasema hayo Ijumaa Mei 13, 2022 alipokuwa akifunga mafunzo ya kijeshi kwa Maafisa na Askari 190 kutoka TFS, TANAPA, NCAA na TAWA katika kambi ya mafunzo ya kijeshi Mlele mkoani Katavi.
” Filamu ile imezinduliwa kwa lengo la kuhamasisha shughuli za utalii na Uwekezaji nchini na tangu izinduliwe kila Mtanzania na Dunia wanafahamu Tanzania kuna nini” amesema Naibu Katibu mkuu huyo.
Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, tangu filamu hiyo izunduliwe inafanya vizuri Kimataifa na tayari Marekani imeoneshwa katika vituo 300 kati ya vituo 355 vilivyoripotiwa kuonesha filamu hiyo.
Amesema mafunzo hayo yakawe chachu ya kuimarisha sekta ya utalii na kuhakikisha Watalii wanapata huduma katika mazingira bora ili kuendana na maono ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amewaeleza Wahitimu hao kuwa wana wajibu wa kulinda misitu, wanyamapori, malikale na vyote ambavyo vinawavutia watalii kuja kutembelea.
” Niwaombe Wahitimu mkatanguliza mbele uzalendo kwa kuhifadhi na kulinda vivutio vyote vya utalii vitakavyokuwa chini yenu, msipotoa huduma nzuri kwa watalii Filamu ya Royal Tour haitakuwa na maana yoyote” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.
Kwa upande wake Mratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Fidelis Kapalata amesema mafunzo hayo waliyoyapata katika yanakwenda kubadili mfumo wao kufanya kazi hususan katika kipindi hiki ambacho ujio wa watalii utakuwa mkubwa kufuatia kuzinduliwa kwa Filamu maarufu ya Royal Tour
Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia – Utawala (SACC-Admn), Luoga Erasto anasema ni matarajio ya Jeshi la Uhifadhi – TFS baada ya mafunzo hayo wahitimu watakwenda kuishi utamaduni wa kijeshi na kuongeza kasi, ufanisi na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa rasilimali za nchi.
“Niipongeze Wizaya ya Maliasili na Utalii kwa kuratibu mafunzo haya yenye lengo la kubadirisha mfumo wa utendaji toka ule wa kiraia na kuwa wakijeshi, sasa taasisi zote za Wizara zinakuwa na mfumo mmoja wa kijeshi ambao utasaidia katika mabadiliko ya kiutendaji,” anasema SACC Luoga.
Katika mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe. Filberto Sanga aliomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia uwezekano wa kuwapangia kazi wilani mwake baadhi ya wahitimu kutoka kila taasisi ya uhifadhi ili waweze kulinda maliasili zilizopo mkoani Katavi kwa kile alichodai mkoa huo umebarikiwa vivutio vingi vya utalii na vingi vikiwa wilayani Mlele.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti