November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa NGOs wahimizwa kutoa maoni mkakati wa kupunguza utegemezi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wadau wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kutoa maoni katika Mkakati wa Mashirika hayo kupunguza utegemezi katika utekelezaji wa miradi na majukumu yao

Rai hiyo imetolewa Mei 12, 2022 jijini Arusha na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa NGOs cha kujadili na kutoa maoni katika Mkakati wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupunguza utegemezi wa wafadhili.

Mhe. Mwanaidi alisema mpaka sasa Kamati imekamilisha andiko la majadiliano (Consultation Paper), nyenzo za ukusanyaji wa taarifa na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali (Stakeholders Engagement Tools), pamoja na ukusanyaji wa taarifa na maoni kutoka kwa wadau na zoezi hilo linaendela katika Kanda ya Kaskazini, Kanda ya nyada za Juu Kusini na Kanda ya Kati.

Mwanaidi aliwataka kuzingatia umuhimu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo na ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla, hivyo alitoa rai kwa washiriki wa mkutano huo kutoa maoni yatakayosaidia kupatikana kwa mkakati huo pia kushirikiana na kamati kwa hali na mali ili kuweza kukamilisha mkakati utakaosaidia kukidhi malengo ya kuanzishwa kwa Mashirika yao na matarajio ya jamii ya watanzania wanayohudumia.

Aidha Mhe. Mwanaidi alisema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamekuwa yakichagiza jitihada za Serikali ili kuwaletea Wananchi wake maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya afua mbalimbali zikiwemo za Afya, Kilimo, Elimu, Maji, Mazingira, Miundombinu, Utawala Bora, Nishati, hifadhi ya Jamii, Mifugo na Uvuvi, Uwezeshaji wa Jamii na Sekta nyingine mtambuka.

”Miradi hiyo, sio tu imewanufaisha Wananchi wetu kijamii, bali pia imechangia katika kuongeza ukuaji wa uchumi, kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza fursa za ajira hususan kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu“alisema Naibu Waziri Mwanaidi

Akitoa taarifa ya Kikosi kazi cha kukusanya maoni juu ya Mkakati wa NGOs kupunguza utegemezi, Katibu Mkuu wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Revocatus Sono alisema Kikosi kazi hicho kimefanikiwa kuwafikia wadau Zaidi ya 700 katika Knda ya Ziwa, Mashariki na Kaskazini hivyo amewahimiza wadau hao kuendelea kushirikiana na Kikosi kazi hicho ili kuapata maoni yatakayosaidia kupata Mkatati huo muhimu kwa ukuaji wa sekta ya NGOs.

Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa NGOs, Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Usajili Mussa Sang’anya alisema Wizara inaendelea na mchakato wa kukusanaya maoni kwa wada katika Kanda mbalimbali kwa kasi ili kufikia malengo yake ya kuwasilisha rasimu ya Mkakati huo kwa Viongozi wa Wizara kwa hatua zaidi za utekelezaji wake.

Kwa upande wake Msajili Msaidizi na Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Arusha Blandina Nkini ameishukuru Wizara kwa kuratibu zoezi hilo ambalo muhimu katika maendeleo ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchuni kwanin itayasaidia kupunguza utegemezi na kuwa na muendelezo wa utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi na majukumu yao.

“Nitoe pongezi kwenu Wizara katika hili hakika mmefanya jambo litakalokumbukwa na vizazi kwa kuweka namna bora itakayosaidia kuokoa NGOs ambazo ufadhili ukipungua au kumalizika zinakosa muelekeo na nyingine zinakufa na kuacha wananchi wakihitaji huduma za NGOs hizo” alisema Blandina

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inashirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kuratibu zoezi la utaoji maoni ya wadau wa NGOs katika kuwa na Mkakati wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupunguza utegemezi na linaendeshwa katika kanda tano za Mashariki, Kati, Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Ziwa.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Kanda ya Kaskazini kilichofanyika jijini Arusha ili kukusanya maoni ya Mkakati wa kupunguza utegemezi kwa NGOs nchini.
Katibu Mkuu wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Revocatus Sona akieleza namna Kikosi kazi cha kukusanya maoni ya Mkakati wa kupunguza utegemezi kwa NGOs nchini katika kikao kilichowakutanisha wadau wa NGOs Kanda ya Kaskazini jijini Arusha
Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Usajili wa NGOs kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mussa Sang’anya akizungumza jinsi Wizara inavyoshirikiana na Baraza la taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika mchakato wa kukusanya maoni ya Mkakati wa kupunguza utegemezi kwa NGOs nchini katika kikao kilichowakutanisha wadau wa NGOs Kanda ya Kaskazini jijini Arusha
Baadhi ya wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Kanda ya Kaskazini wakijadiliana katika kikao cha kutoa maoni kuhusu Mkakati wa kupunguza utegemezi kwa NGOs nchini kilichofanyika jijini Arusha