November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB yaungana na waislamu Tanga kupata futari ya pamoja

Na Hadija Bagasha Tanga,

Benki ya NMB imetenga asilimia moja ya mapato kwa ajili ya kufanikisha huduma za kijamii na kutumia kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu, ujenzi wa madarasa na ukarabati wa majengo mbalimbali pamoja na kutoa misaada kwenye matukio ya maafa.

Katika mwezi huu mtukufu wa ramadhani Benki hiyo imeungana na waumini wa dini ya kiislam Mkoani Tanga kwa lengo la kupata futari ya pamoja baada ya kubaini kuwa
ufanisi wa Benki hiyo unatokana na wananchi wake.

Hayo yamesemwa na Said Pharseko Mwakilishi wa meneja wa kanda ya Kaskazini wakati alipokuwa akizungumza katika hafla ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na benki hiyo jijini hapa.

Alisema benki hiyo ni ya wananchi hivyo wameona ni vyema wanachokipata kama faida kwao wakaungana pamoja na kupata futari ya pamoja na waislamu mbalimbali katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

‘’Kama mnavyoafahamu kwamba benki ya NMB ni moja ya benki inayofanya shughuli zake hapa Mkoani Tanga na nchi nzima kwa ujumla washiriki wake wakubwa ni wananchi kama tunavyofahamu huu ni mwezi mtukufu wa ramadhani sisi kama benki ya NMB tumeamua kufanya tukio hili la kufuturisha ili kuunganika na waislamu wote hapa Mkoani Tanga,’’alisema Mwakilishi wa meneja huyo wa kanda.

Aliongeza kuwa ufanisi wa benki hiyo unatokana na wananchi na wananchi wenyewe ndio hawa hivyo tumeona ni vyema ile faida tunayoipata kwao tufanye tukio la kufuturisha tunawashukuru sana kwa kushirikiana nasi kwani bila wao sisi tusingekuwepo mahali hapa,’’Alisema Said Pharseko

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa aliwataka waislamu wote Nchini kuongeza nguvu zaidi katika kuwaandaa na kuwalea vijana wa kiislamu kwa kufuata misingi na taratibu za dini inavyowataka kwa lengo la kuwaepusha kujiingiza katika matendo maovu pamoja na makundi yasiyofaa.

Sanjari na hayo Mgandilwa aliwataka waumini wa dini ya kiislamukushirikiana na kuungana pamoja na waumini wa dini ya kikristo katika kuhakikisha wanadumisha amani ya Taifa na Nchi nzima kwa ujumla.

Kwa upande wake Meneja wa benki ya NMB tawi la Tanga Elizabeth Chawinga ambaye ni meneja wa benki hiyo Mkoani Tanga aliwataka wakazi wa Tanga kuendelea kutumia benki hiyo wakiamini ni mkombozi kwa maisha yao.

“Hivi karibuni tunatarajia kuzindua tawi jingine la benki yetu ya NMB pale kwenye ofisi za ccm Mkoa lengo la kufanya hivyo ni kusogeza huduma zetu karibu kabisa na wananchi tunaomba muendelee kutuamini na kutumia huduma zetu, “amesisitiza Chawinga.

Baadhi ya wateja wa benki hiyo akiwemo Yakub waliishukuru NMB kwakuwaandalia futari hiyo na kuziomba Taasisi na mashirika mengine kuiga mfano wa kuwakutanisha waislamu pamoja kama ilivyofanya NMB benki.