Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa huduma ya uchunguzi wa kimaabara ni muhimu kwa ajili ya utoaji wa matibabu sahihi na bora kwa wagonjwa na hupunguza gharama zisizo za lazima.
Hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo watumie fursa ya maadhimisho ya wiki ya huduma za maabara Mkoa yatakayofanyika Mei 2-6 mwaka huu katika viwanja vya Furahisha wilayani Ilemela,wajitokeza na kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.
Pamoja na kupatiwa elimu juu ya matumizi sahihi ya huduma za maabara na shughuli mbalimbali zinazofanya na wanataaluma wa sayansi za afya nchini.
Mhandisi Gabriel,ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza,juu ya maadhimisho hayo ambayo yameandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Chama Cha Wanasayansi wa Maabara za Afya Taifa(MeLSAT) yatafanyika kwa siku 5 mkoani hapa yenye kauli mbiu “vipimo vya maabara za afya ndio msingi wa matibabu bora,kazi iendelee.
“Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanahitaji damu katika hospitali zetu,wengi wao wakiwa ni watoto chini ya miaka 5,wakina mama, wajawazito,watu wenye magonjwa sugu na wanaopatwa na ajali,” amesema Mhandisi Gabriel.
Amesema,maadhimisho ya wiki ya huduma za maabara hufanyika ulimwenguni kote kila mwaka mwishoni mwa mwezi April,kwa hapa nchini maadhimisho haya ni ya 13 na kimkoa ni ya kwanza kufanyika.
Ambayo yatakwenda sambamba na utoaji wa huduma mbalimbali bila malipo ikiwemo kupima na kutambua magonjwa ya kisukari, malaria,kaswende,shinikizo la damu,virusi vinavyosababisha magonjwa ya VVU, hepatitis B na C.
Kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya huduma za maabara na shughuli mbalimbali zinazofanywa na wanataaluma wa sayansi za afya nchini, uchangiaji wa damu,kutoa elimu juu ya shughuli za Baraza la Wataalamu wa Maabara,maonesho ya vifaa mbalimbali vya maabara,kupima viashiria vya saratani ya tezi dume na kutoa ushauri.
Pia ametoa wito kwa waajiri wote ndani ya Mkoa wa Mwanza kuwaruhusu wataalamu wa maabara ili washiriki kikamilifu katika tukio hilo muhimu la kitaaluma na bila kuathiri utendaji wa kazi katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa MeLSAT Mkoa wa Mwanza Bertrand Msemwa amesema,lengo la kuandaa maadhimisho hayo ni kwa ajili ya kujenga na kukuza uelewa wa wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya zao.
Amesema,jambo kubwa wananchi wanapaswa waelewe bila kipimo maabara,bila kufanyiwa uchunguzi walienda kupata dawa maana yake wanaenda kuharibu afya zao lakini pia wanasababisha shida na kuingia katika gharama ambazo hazina msingi wowote.
Hivyo wanawashauri wananchi waweze kufanya vipimo na kupata ushauri wa kitaaluma kabla ya kuanza kutumia dawa hii itasaidia kupunguza madhara yalipo sasa tatizo lililopo dunia nzima la suala la usugu wa dawa ambalo linaendana na tabia ya wananchi kutumia dawa bila kufuata utaratibu wa vipimo.
“Lengo moja wapo ni kuhakikisha wananchi wanaelewa majukumu ya maabara,wanafanya nini na wanahusika vipi katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama katika afya zao,maabara inahusika katika utoaji wa vipimo na kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ya magonjwa ya binadamu na tunaweza kutoa majibu bora kwa ajili ya kusaidia matibabu,”amesema Msemwa.
More Stories
Tanzania yapanda viwango Utawala wa Sheria Duniani
Rais Samia apeleka neema Tabora
Samia apeleka neema Tabora, aidhinisha Bil. 19/- za umeme