November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCBRT, Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete kuchangisha fedha kuendesha Kitengo kipya cha Mama na Mtoto

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya chakula Cha usiku iliyoandaliwa na hospitali ya CCBRT kupitia Kitengo chake kipya cha Afya ya uzazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete, kwaajili ya kuchangisha fedha zitakazotumika kutoa huduma ya uzazi salama kwenye Kitengo cha Afya ya uzazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT Brenda Msangi alisema lengo la hafla hiyo ambayo itafanyika Mei 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni kutatua changamoto zinazowakabili wakina mama wajawazito walioko katika mazingira magumu na uzazi hatarishi.

Brenda alisema hospitali ya CCBRT kwa kushirikiana na serikali wamekuwa wakitoa huduma ya afya ya uzazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam ili kujenga uwezo wa wataalamu wa Afya walioko kwenye vitengo vya Afya ya uzazi katika hospitali za umma za mkoa wa Dar es Salaam;

“Ingawa Kitengo hiki tunategemea kufunguliwa rasmi mwezi Juni, tumeanza kutoa huduma kwa awamu tokea mwezi januari na kufikia sasa tumezalisha akina mama wajawazito wapatao 37. Kitengo hiki kitatumika kama hospitali ya rufaa ya kanda na tutakapoanza kutoa huduma kwa ukamilifu wake tutakuwa na uwezo wa kuwahudumia akina mama wenye ujauzito hatarishi wapatao 12,000 kwa mwaka”

Aidha Brenda alisema Kitengo hicho Cha Afya ya uzazi kina miundombinu maalum ya kuwahudumia wanawake wajawazito wenye Ulemavu, wenye historia ya fistula na mabinti wanaopata ujauzito wakiwa na umri mdogo ili kuhakikisha wanawake wote wanapata huduma ya uzazi salama hivyo kupitia Kitengo hicho wana dhamira ya kuunga juhudi za serikali za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi sambamba na Kuzuia ulemavu.

Mbali na hayo, Brenda alisema, CCBRT inatambua kuwa Kinga huleta matokeo mazuri ya muda mrefu kuliko tiba na kwamba uzazi salama huzuia Ulemavu wa maisha kwa sababu hiyo mwaka 2010 CCBRT kwa kushirikiana na timu ya Afya ya mkoa wa Dar es Salaam na Manispaa zake tano walianza kutoa huduma Pana za Afya katika mifumo ya afya ya uzazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam tangu wakati huo hadi sasa wameweza kuvifikia vituo vya Afya na hospitali 23 za Umma mkoani humo;

“Kwa sasa vituo hivi vina vifaa tiba na maboresho yamefanyika kwenye miundombinu kuongezeka kwa utendaji kazi na hivyo kuwezesha huduma salama na zinazofikika kiurahisi kwa akina mama na watoto”

Brenda aliongeza kuwa “Mifumo ya Rufaa imeimarishwa ili kupunguza msongamano hasa kwenye hospitali kubwa, vituo vinakusanya takwimu sahihi na zenye ubora kwa kutumia mifumoya kisasa kama vile mpango wa kutambua changamoto za vifo vya watoto wachanga”

Brenda amewaomba wadau wote wa Afya ya uzazi kuwaunga mkono ili kuwezesha mazingira ya uzazi yaliyo salama, yenye staha na ubora kwa mama zetu na kwamba ifike siku moja kila mwanamke aweze kutarajia ujauzito na kujifungua salama, heshima na Kwa furaha

Kwa upande wake Meneja wa Mawasiliano kutoka Kampuni ya Coca-Cola Kwanza, Victor A Byemelwa ametoa wito kwa watanzania wenye moyo wa kusaidia jamii kuchangia ili kufanikisha uendeshaji wa kitengo kipya cha mama na mtoto kitakachotoa huduma katika Hospitali ya CCBRT.