Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amewapongeza TANROAD kwa hatua walizochukuwa kumsimamia Mkandarasi kutoka kampuni ya SINOHYDRO anaetekeleza Awamu ya pili ya mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mabasi ya mwendokasi Kilwa road.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua Miradi ya maendeleo Wilaya ya Temeke, RC Makalla amefurahi kuona Ujenzi huo umefikia Asilimia 52 ambapo amemtaka Mkandarasi kuongeza bidii ili kazi ikamilike kabla ya mwezi March mwakani ili lengo la Rais Samia Suluhu Hassan kutoa huduma bora ya usafiri iweze kutimia.
Kutokana na mwenendo Mzuri wa Mkandarasi, RC Makalla ameelekeza kuwepo kwa utaratibu rafiki utakaofanya Shughuli za Ujenzi zinazoendelea zisiathiri Shughuli za Wananchi ikiwemo kusababisha foleni, vumbi na hata kuzuia uzalishaji viwandani.
Hata hivyo RC Makalla amewaelekeza TANROAD na TARURA kumpatia taarifa ya mgawanyo wa Majukumu yao hususani kuweka makubaliano ya nani anapaswa kusimamia Mifereji na Mitaro.
Katika ziara hiyo RC Makalla pia ametembelea Ujenzi wa Zahanati ya Toangoma inayogharimu Shilingi Milioni 250 na Zahanati ya Kilakala inayogharimu Shilingi Milioni 250 ikiwa ni fedha zitokanazo na Tozo za Simu ambapo amepongeza Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa kusimamia kikamilifu Miradi ya maendeleo.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia