November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu 6 wafariki dunia, 19 wajeruhiwa kwa ajali ya gari Tanga

Na Hadija Bagasha Korogwe,

Watu sita wamefariki dunia na wengine 19 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka katika eneo la Kwamduru wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo gari aina ya Coaster yenye namba za usajili T833 DMH kuacha njia na kupinduka.

Kamanda Jongo alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magunga wilayani Korogwe na majeruhi wanaendelea kupata matibabu hospitalini hapo.

“Waliofariki ni wanawake watatu na wanaume watatu ambapo katika hao wanawake mmoja ni mtoto anayekadiriwa kuwa na miaka mitatu ambaoi maiti watano wametambuliwa na ndugu zao mmoja bado hajatambuliwa,” alibainisha Kamanda Safia.

Aidha, Kamanda Jongo alieeleza kuwa gari hiyo ilipokaguliwa ilionekana ina vibali vya kukodishwa kutokea Dar es Salaam kuelekea kilimanjaro na kwamba abiria hao walikuwa wanakwenda msibani mkoani Kilimanjaro.

“Dereva wa gari hiyo ni mmoja wa majeruhi na yupo chini ya uangalizi kutokana na kubainika kufanya udanganyifu katika vibali vya gari hilo,” amesema.

“Baada ya ajali kutokea na kufanya mahojiano ya kina na abilia wakili kwamba pale mbezi walikatiwa tiketi na kwamba walidanganya kuwa wamekodi “

Aidha chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa ni mwendo kasi aliokuwa nao dereva na kusababisha kushindwa kukata kona na gari kutelezaa kisha kupinduka.

Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Jongo ametoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto barabarani kufuata sheria ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.

Mohamedi Shabani ni miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo alieleza chanzo cha ajali kuwa kulikuwa na mvua eneo hilo na kwamba gari iliteleza na kupinduka.

” Ilikuwa usiku wa saa tisa tunatokea dar na kuelekea kilimanjaro kwenye mazishi sasa mvua imesababisha uteleza na mbele kulikuwa na kona kali na daraja ndio gari ikanduka dereva hakuwa katika mwendo mkali ni kuteleza ” alibainisha Mohamedi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Dk Salma Swedi amethibitisha kupokea miili sita na majeruhi 19 na kuongeza kuwa majeruhi wawili hali zao ni mbaya na wanatarajiwa kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo.

Gari aina ya Coster iliyopata ajali wilayani Korogwe Mkoani Tanga. Picha na Hadija Bagasha Tanga.